WABUNI INJINI ISIYOTEGEMEA MAFUTA KUJIENDESHA.

 Shukuru Machupa na David Ng’unda wakiwa wameshikilia kifaa hicho.

Peter Akaro

KATIKA kupambana na kuhakikisha sayansi inaleta unafuu wa kimaisha, vijana wawili kutoka chuo cha st. Joseph Dar es Salaam wamefanikiwa kubuni kifaa (injini) walichokipa jina la ‘Green Energy Heat Exchanger’ kama nishati mbadala isiyoharibu mazingira.

Ni David Ng’unda na Shukuru Machupa wanaeleza kuwa kifaa hiki ni aina ya injini ndogo yenye kutumia mfumo wa ubadilishaji wa joto la hewa au gesi ambayo hupatikana ndani ya silinda (heat exchanger).

Joto hilo linaweza kutokana na chanzo chochote kama vile jua, moto, maji ya moto, au hewa ya moto kutoka kwenye mashine nyingine.

Kifaa kinaweza kuunganishwa na mifumo mbalimbali ya kiutendaji katika kuzalisha nishati ya umeme, mifumo hii ni kama ule wa bio ges, mfumo wa kutumia mvuke, mifumo yote hii inatoa majibu chanya katika uwezeshaji wa mashine hii kufanya kazi kwa ufanisi zaidi na kutoa msukumo zaidi katika ufanyaji kazi wake.

Hivyo basi, injini huweza kujiendesha bila kutengemea nishati kama mafuta, na yule mwenye kifaa hicho huweza kukitumia kwa matumizi mbalimbali.

UFANYAJI KAZI WAKE.

Injini inaweza kutumia hewa ya kawaida au gesi aina ya hydrogen au helium ambazo huwekwa ndani ya silinda bila ya kuachiwa huru (silinda huzibwa pande zote), hakuna hewa inayoruhusiwa kutoka au kuingia ndani ya silinda kama inavyofanyika katika injini nyingine.

Machupa anasema injini hii haitaji ‘valve’ ambayo huruhusu mafuta kupita au lah, kuingia na kutoka kwa hewa, na pia haina uchomaji wa ndani kama vile injini za petrol au diesel.

Kama zilivyo injini nyingine, hii nayo pia inayo mizunguko minne katika ufanyaji kazi wake, kwanza ni upoozaji, ubanaji, uchomaji, na utanukaji ambapo vitendo hivi ufanyika wakati injini hiyo ikifanya kazi.

Mabadiliko ya joto ndani ya silinda ambayo hutokana na vyanzo vyovyote vilivyotajwa hapo awali hufanya silinda kutanuka, hewa hiyo ya moto ndio itafanya msukumo mkubwa wa injini, hivyo basi kupata mzunguko endelevu hewa au gesi hiyo inahitaji kupozwa ili kupata mzunguko kamili.

Anasema Upozaji wa hewa au gesi hiyo unaweza kuwa wa maji au wa kawaida (bila ya maji), kutokana na tabia ya hewa kutanuka inapopata joto kali na kurejea katika hali yake ya kawaida inapopoa, hivyo basi injini hii inatumia mfumo huo wa utanukaji wa hewa na upozaji wake kufanya kazi.

“Kupata mzunguko ulio kamili na endelevu ndani ya silinda utafanya pistoni kupanda au kushuka kwa msaada wa kifaa cha ubadilishaji (displacer) ambacho ufanya hewa kwenda chini au juu kwa ajili ya kupata joto au kupozwa, pia pistoni inaungwa kwenye shafti kama injini nyingine.

“Muhimu kuzingatia mzunguko wa piston na kifaa cha ubadilishaji katika ufanyaji kazi wa injini, ni mpishano wa vitu hivyo viwili ni lazima uwe wa digrii 90,” anasema Machupa.


 Injini inatumia magurudumu ya kuelea (flywheel) kusaidia kupata mzunguko mzuri na wenye kasi nzuri, pia inaweza kuungwa katika kitu ambacho kinahitaji mzunguko mfano pampu za maji au hata jenereta kutokana ukubwa na mahitaji ya injini na kifaa kinachosukuma.

  Injini inayojiendesha kwa kutengemea hali ya hewa.

VIFAA VILIVYOTUMIKA KUITENGENEZA.
Silinda ambayo inaweza kuwa zaidi ya moja, pistoni (kwa hapa imetumia malighafi yenye kutanuka aina ya raba kama pistoni), flywheel pamoja na shafti, displacer (kifaa cha ubadilishaji), mbao kwa ajili ya umbo na mshumaa au kibatari kama chanzo cha joto.

FAIDA ZAKE KATIKA JAMII.

Machupa anasema injini inaweza kutumika kuvuta maji katika visima vijijini na sehemu zenye shida ya kupata nishati ya umeme, hivyo ni rahisi kufua umeme bila ya tatizo kutokana na vyanzo vyake vya uendeshaji vinapatika nchi nzima.

“Injini haitaji vifaa ambavyo ni gharama na upatikanaji wake ni wa shida, hivyo unaweza kutumia vifaa vya manyumbani.

“Pia injini ni rafiki kwa mazingira, unaweza kutumia bio gesi ambayo hutokana na kinyesi cha wanyama au nishati ya jua bila ya kuchafua mazingira,” anasema mbunifu huyo.

kwa sehemu za vijijini umeme utakuwa wa kutosha kulingana na matumizi yao, kwa upande wa kampuni za uzalishaji umeme injini hii inaweza kuongeza upande za joto taka inayotoka kwenye mashine za uzalishaji ili kuongeza nguvu ya upatikanaji wa umeme.

Anaongeza kuwa kifaa hiki wanategemea kuwa mkombozi kwa jamii zisizofikiwa na umeme hasa katika shule za serikali za mabweni katika kuwawezesha kupata nishati ya umeme kwa gharama nafuu.

USHAURI KWA SERIKALI.

Shukuru anaishauri serikali kuwajenga vijana katika kutatua matatizo yao katika jamii, ubunifu kama huu usichukuliwe kwa madhumuni ya maonyesho bali ufanyiwe kazi na kutumia vijana katika nyanja husika ni kuleta tija kwa taifa katika maswala ya kisayansi na ubunifu.

 “Ni vema Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi kutumia nguvu kubwa katika kuwaandaa vijana kwa ngazi ya sekondari kupitia wadau wanaoonyesha nia ya ya dhati ya kuwasaidia vijana wabunifu. 

“Vijana tuko tayari kufanya kazi na mtu yeyote ambaye ataona umuhimu wa ugunduzi huu na hatutoishia hapa katika kuleta tofauti katika jamii na kusaidia watanzania katika kutatua shida zao kwa kutumia elimu yetu na ukuaji mzima wa sayansi na teknolojia,” anasema.

Hii ni  injini inayojiendesha kwa kutengemea hali ya hewa.

WASIFU WA WABUNIFU.

Shukuru Mchupa na David Ng’unda ni vijana wa kitanzania ambao ni wanafunzi wa mwaka wa pili katika Chuo cha st Joseph ambapo wanasomea uhandisi wa mitambo (Mechanical Engineering).

Ng’unda elimu yake msingi aliipata Bethel Mission, na sekondari kwa vidato vyote alisoma Loyola high school.

Machupa alisoma shule ya msingi Olympio, na elimu yake ya sekondari aliipata Lord Baden Powell memorial high school, na kidato cha tano na sita alisoma Pugu high school.

Comments

Post a Comment

Popular posts from this blog

SERIKALI YAREJESHA KAMBI TANO ZA JKT ZILIZOKUWA ZIMESITISHA MAFUNZO YA JESHI.

BELENG’ANYI, MBUNIFU MWENYE MALENGO YA KUTENGENEZA MGODI WA KUFUA UMEME.

WAKULIMA WA ZAO LA VITUNGUU IRINGA WATELEKEZA MASHAMBA.