UTAFITI WA VIASHIRIA NA MATOKEO YA UKIMWI WA MWAKA 2016/17 KUFANYIKA DAR ES SALAAM
Na: Veronica Kazimoto
Dar es Salaam
05 Mei, 2017.
UTAFITI WA VIASHIRIA NA MATOKEO YA UKIMWI WA MWAKA 2016/17 KUFANYIKA DAR ES SALAAM MWISHONI MWA MWEZI MEI, 2017
Wito umetolewa kwa Wananchi wote wa Mkoa wa
Dar es Salaam ambao kaya zao zimechaguliwa kitaalam kwa ajili ya Utafiti wa Viashiria na Matokeo
ya UKIMWI wa mwaka 2016/17 kutoa ushirikiano kwa wadadisi wataokusanya taarifa
za utafiti huo utakaofanyika mwishoni mwa mwezi Mei, mwaka huu.
Akizungumza hivi karibuni katika Mkutano wa Wadau wa Utafiti huo jijini
Dar es Salaam, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema alisema, Utafiti huo ni
muhimu sana kwani husaidia kujua hali halisi ya ugonjwa wa UKIMWI na hivyo
kuongeza nguvu zaidi ya kuondokana na ugonjwa huo.
"Mimi niwaeleze tu kwamba, utafiti huu
ni muhimu sana katika Mkoa wetu wa Dar es Salaam kwa kuwa utatusaidia kujua
hali halisi ya maambukizi ya VVU na hatimaye kupata nguvu zaidi za kuondokana
na ugonjwa huu, hivyo nawaagiza kusimamia zoezi hili na kuwahimiza Wananchi
wote ambao kaya zao zimechaguliwa kutoa ushirikiano kwa wadadisi watakaofanya
taarifa za utafiti huu", amesema Mjema.
Mjema amefafanua kuwa, utafiti huu ni wa
kwanza kukusanya taarifa zinazohusiana na maambukizi mapya ya VVU, kiwango cha
VVU mwilini kwa watu wanaoishi na VVU na wastani wa maambukizi ya VVU kwa watu
wa rika zote pamoja na wingi wa chembechembe za kinga mwilini (CD4 T-cell
count).
Aidha, utafiti huu utapima uwepo wa viashiria
vya usugu wa dawa, kiwango cha maambukizi ya kaswende pamoja na homa ya ini
(Hepatitis B).
Akizungumzia kiwango cha maambukizi ya VVU
katika tafiti zilizopita, Mkuu wa Wilaya huyo ameeleza kuwa, maambukizi
yamepungua kutoka asilimia 7 mwaka 2003 mpaka asilimia 5.1 mwaka 2011 na
kuifanya Tanzania kuwa ni miongoni mwa nchi zenye kiwango cha chini cha
maambukizi ya nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara ambapo nchi nyingi za ukanda
huo zina kiwango cha zaidi ya aslimia 10.
Nae, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Dkt. Grace
Magembe amesema kuwa, kwa mkoa wa Dar es Salaam, utafiti huu utahusisha kaya zisizozidi
1,000 na Wananchi watakuwa na hiari ya kukubali kupima ambapo kwa wale
watakaogundulika kuwa na maambukizi, watapata rufaa ya kwenda kupatiwa matibabu
bure katika vituo vya kutolea huduma za afya.
"Utafiti huu wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI hauhusishi
watu wote bali ni kaya chache tu
ambazo zimechaguliwa kitaalam ili ziweze kuwakilisha kaya nyingine na kwa hapa
Dar es Salaam kaya zilizochaguliwa hazizidi 1000", amesema Dkt. Magembe.
Utafiti wa aina hii ni wa mara ya nne (4) kufanyika
nchini Tanzania ambapo wa kwanza ulifanyika mwaka 2003, wa pili mwaka 2007 na
wa tatu mwaka 2011.
Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania wa
mwaka 2016 /17 unafanyika nchini, chini ya usimamizi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa
kushirikiana na Wizara ya Afya kwa Tanzania Bara, Wizara ya Afya Tanzania
Zanzibar, Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar (OCGS), Tume ya Taifa ya
Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) na Tume ya UKIMWI Zanzibar (ZAC).
Mkuu wa Wilaya ya Ilala ,Sophia Mjema akizungumza hivi karibuni na Wadau waUtafiti wa Viashiria na Matokeo ya
UKIMWI Tanzania wa mwaka 2016/17. Kwa Dares Salaam, utafiti huu unatarajia kuanza mwishoni mwa mwezi Mei,
2017.
Baadhi ya Washiriki waliohudhuria Mkutano wa Wadau wa Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania wa mwaka
2016/17 uliofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Msahauri, Dkt. Cecilia
Makafu kutoka Shirika la ICAP Tanzania akiwasilisha mada kuhusu Utafiti wa
Viashiria na Matokeo ya UKIMWI wa mwaka 2016/17 kwa wadau wa Utafiti huo wa
Mkoa wa Dar es Salaam.
Comments
Post a Comment