CHAMA CHA SKAUTI TANZANIA KUADHIMISHA MIAKA 100 JULAI 21 HADI 28 MWAKA HUU.

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

CHAMA cha Skauti Tanzania kinatarajia kuadhimisha miaka 100  ifikapo Tarehe 21 hadi 28 Julai  Mwaka huu  katika Kampasi ya Chuo Kikuu Makao Makuu Mjini Dodoma.

Aidha Vijana wapatao 5,000 kutoka Wilaya zote za Tanzania Bara na Zanzibar pamoja na zaidi ya wageni 1,000 kutoka Nje ya Tanzania wanatarajiwa kushiriki maadhimisho hayo.

Taarifa iliyotolewa jana kwenye vyombo vya habari  na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Othman Khamis Ame inasema kuwa Mkuu wa Skauti Tanzania, Mwatum Mahisa alieleza hayo alipokuwa  akiuongoza Ujumbe wa Viongozi  Tisa wa Chama hicho Bara na Zanzibar alipokuwa akitoa Taarifa hiyo kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Vuga Mjini Zanzibar.

 Mwatum, alisema vugu vugu la maadhimisho hayo limekuja kufuatia ziara ya Waziri Mkuu Mstaafu wa Tanzania wa Awamu ya Nne Mizengo Peter Pinda alipofanya ziara ya kuhudhuria maadhimisho ya Skauti Nchini Uganda Mwaka 2016.

Alisema kutokana na uzito wa maadhimisho hayo Kitaifa yatakayo ambatana na maonyesho  mbali mbali  na Tuzo maalum zitatolewa kwa Marais waliopita pamoja na watu waliofanya ushujaa zaidi katika utekelezaji wa  ujenzi wa Taifa kiuzalendo.

Mkuu huyo wa Skauti Tanzania alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba mipango imeanza kuchukuliwa katika hatua za awali za maadhimisho hayo ambapo Vijana  Kumi wa Skuli za Msingi na Kumi Sekondari wataandaliwa kila Halmashauri za Wilaya Nchini  kwaajili ya kushiriki kwenye tukio hilo muhimu.

Alieleza kwamba Wizara za Elimu, Afya, Mambo ya Ndani, Mambo ya Nje, Tamisemi pamoja na ile inayosimamia Utamaduni kwa upande wa Tanzania Bara zimeshateuliwa  na Waziri Mkuu  Kassim Majaliwa  kusimamia  jambo hilo la Kihistoria.

Mwatum alifahamisha kwamba Mataifa Manne ya Kigeni ambayo ni Korea, Poland, Uganda, na Malawi yameshathibitisha kuhudhuria Maadhimisho hayo.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haina pingamizi kwa Vijana wake katika kushiriki Maadhimisho hayo ya Miaka 100 ya Skauti Tanzania.

Balozi Seif alisema Skauti ni sehemu muhimu na adhimu kwa kuwaandaa Vijana katika muekeo wa kuwa na Utii, Heshima na Maadili mema, lakini kubwa zaidi ni kujengeka katika mazingira ya kuwa Wazalendo kwa Taifa lao.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kati kati akisalimiana na Uongozi wa Skauti Tanzania alipokutana nao kwa mazungumzo kumtaarifu maandalizi ya maadhimisho ya kutimia Miaka 100 ya Skauti Tanzania yanayotarajiwa kufanyika Makao Makuu Mjini Dodoma.


 Balozi Seif akizungumza na Uongozi wa Skauti Tanzania hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar jana.


 Mkuu wa Skauti Tanzania, Mwatum Bakari Mahisa akitoa Taarifa za maadhimisho ya kutimia miaka 100 tokea kuanzishwa kwa Chama cha Skauti Nchini Tanzania.

 Balozi Seif  kati kati waliokaa vitini akiwa katika picha ya pamoja na Uongozi wa Skauti Tanzaania mara baada ya kumaliza  mazungumzo yao, wa kwanza kulia ni Kamishna Mkuu wa Skauti Tanzania Ndugu Abdulkarim Shah.


 Balozi Seif akibadilishana mawazo na kuagana na Skauti Mkuu Tanzania  Mwatum Makari Mahisa Nje ya Ofisi yake Vuga Mjini Zanzibar.


Balozi Seif  akiagana na Kamishna wa Skauti Zanzibar  ambae pia ni Katibu Mkuu Mstaafu wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Maalim Ali Rajab.
           (PICHA ZOTE NA OMPR –ZNZ)

Comments

Popular posts from this blog

SERIKALI YAREJESHA KAMBI TANO ZA JKT ZILIZOKUWA ZIMESITISHA MAFUNZO YA JESHI.

BELENG’ANYI, MBUNIFU MWENYE MALENGO YA KUTENGENEZA MGODI WA KUFUA UMEME.