MAABARA SABA ZA UCHUNGUZI WA MAGONJWA YA BINADAMU MKOANI IRINGA ZAFUNGIWA.

Na Mwandishi Wetu, Iringa.

BODI ya Usajili na Usimamizi wa Maabara Nchini imezifungia maabara saba za uchunguzi wa magonjwa ya binadamu zilizopo katika Halmashauri mbalimbali mkoani Iringa kwa kukiuka taratibu za uendeshaji huduma hizo ikiwamo kutumia wataalamu wasio na sifa jambo linalokiuka sheria namba 10 ya uanzishwaji na uendeshaji wa maabara ya mwaka 1997.

Akizungumza mjini Iringa jana Kaimu Mkaguzi wa Bodi hiyo, Ednanth Gareba alisema bodi hiyo imekagua maabara zaidi ya 40 na kubaini mapungufu makubwa kwenye maabara hizo ambapo asilimia 50 ya maabara zilizokaguliwa  zilikuwa hazijakidhi vigezo vya kutoa huduma hiyo.

Gareba alisema kuwa wao kama serikali wanachohitaji ni huduma bora kwa watanzania wote na sio huduma, wanavyofungia maabara hizo wameona hakuna namna nyingine ya kufanya tofauti na kufunga kwa sababu hawana watalamu.

Naye Ofisa Utawala Kituo cha Afya Nyololo, Diana Yesaya ,alisema baadhi ya wamiliki na wasimamizi wa vituo vya afya na maabara wanashindwa kukamilisha ushajili kutokana na  gharama kubwa ya ukamilishaji taratibu za usajili wa maabara pamoja na wahudumu wake ni moja ya sababu ya baadhi ya wamiliki kushindwa kufuata taratibu.

Hata hivyo, wameiomba bodi hiyo kuwatazama wananchi wenye mahitaji ya huduma hizo.

Kwa upande wake,  Mratibu na Msimamizi wa Maabara Mkoa wa Iringa Frank Mugoba, alisema serikali inatambua umuhimu wa maabara hizo hasa zile zinazotoa huduma katika maeneo ya vijijini lakini ukiukwaji wa taratibu ikiwamo kuajiri wahudumu wasio na ujuzi hitajika si suala la kufumbiwa macho.


Comments

Popular posts from this blog

SERIKALI YAREJESHA KAMBI TANO ZA JKT ZILIZOKUWA ZIMESITISHA MAFUNZO YA JESHI.

BELENG’ANYI, MBUNIFU MWENYE MALENGO YA KUTENGENEZA MGODI WA KUFUA UMEME.