WAKULIMA WA ZAO LA VITUNGUU IRINGA WATELEKEZA MASHAMBA.
Na Mwandishi Wetu, Iringa
BAADHI ya wakulima wa zao la vitunguu wilayani
Iringa wamelazimika kutelekeza na kuacha kuhudumia mashamba yao kutokana na
kukosa masoko ya uhakika hali ambayo imewaathiri kiuchumi, kisaikolojia na
kuuwa mitaji yao.
Wakizungumza na mwandishi wa blog hii, mashambani
huko yaliyopo eneo la Kiwere wilayani Iringa wakulima hao ,walisema pamoja na kuacha kuhudumia mashamba yao bado
wanailalamikia serikali kuweka ushuru mkubwa wa kodi ya mazao kwenye mageti
pamoja na wanunuzi kutaka wakulima hao wauze mazao yao kwa lumbesa.
Idhaa Ally
alisema kutokana na changamoto hizo
wakulima wengi wameathirika kiuchumi na kisaikolojia kutokana na wengi wao
kukopa fedha benki kwa ajili ya kilimo.
“Sisi tunatumia gharama kubwa kuanzia kuandaa shamba
hadi kuvuna lakini changamoto inakuja kwenye soko na ukiangalia wengi wetu
wakulima tumechukua mikopo na tunashindwa kurudisha kutokana na mazao
kutonunulika.”alisema Ally.
Naye, Chacha Omary alisema pembejeo za kilimo zimekuwa gharama kubwa sana kiasi cha wakulima wadogo kushindwa kumudu gharama hizo.
Hata hivyo Omary aliiomba serikali kupunguza gharama za pembejeo za kilimo ili wakulima wadogo waweze kumudu gharama za pemebejeo hizo.
Elizabeth Chilala ambaye amelima hekari mbili alisema ametumia zaidi ya Sh. Mil.4.5 lakini ameambulia kupata magunia 70 tu hali ambayo imemkatisha tamaa ya kuendelea kulima zao hilo kutokana na gharama za uendeshaji kuwa kubwa.
Chilala alisema matarajio yake alikuwa auze gunia moja kwa sh.100,000 hadi 150,000 lakini hali imekuwa tofauti na kulazimika kuuza kwa gunia moja kwa sh. 50,000.
Ofisa Kilimo wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Lucy Nyalu alikiri changamoto hiyo na kusema wao kama serikali wanawahamasisha wakulima kulima kilimo cha kibiashara ili kujihakikishia kuwa na kipato pamoja na chakula cha uhakika.
Mkurugenzi Mtendaji wa
Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Vijijini, Robert Masunya, alisema Halmashauri inatambua masuala ya lumbesa na
pia inatambua sheria ya wakala wa vipimo ya mwaka 2002 sura ya 340
ambayo inatoa mwelekeo mzima juu ya usimamizi wa mazao kwa kuzingatia uzito.
PICHA KWA MSAADA WA MTANDAO
Comments
Post a Comment