VIONGOZI WA DINI YA KIISILAMU WAOMBWA KUTOTOA HIFADHI KWENYE NYUMBA ZA IBADA.
Na Mwandishi Wetu, Kilolo.
SERIKALI mkoani Iringa imewaomba viongozi
wa dini ya kiislamu kutowaruhusu watu wasiowafahamu kuwapa hifadhi kwenye nyumba zao za
ibada na badala yake wawape hifadhi watu wanaowafahamu ili kutowapa nafasi
wanaoitumia dini hiyo kwa uovu.
Kauli hiyo imetolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza wakati akizungumza na viongozi
mbalimbali wa serikali,madhehebu ya dini kutoka kona zote za mkoa wa Iringa na
wananchi wengine ambao walijumuika kwa pamoja kwenye hafla ya chakula cha jioni
(futari) kilichoandaliwa na halmashauri ya wilaya ya Kilolo mkoani Iringa.
Masenza alisema
kuna baadhi ya maeneo kumeibuka
tabia ya watu kutumia kigezo cha dini kufanya vitendo viovu ikiwamo utapeli na
uasi jambo linalolenga kuchafua dini ya uislamu.
“Niwaombe viongozi wangu wa dini msitumie kipindi hiki
cha mfungo kuwaruhusu watu msiowafahamu kulala kwenye nyumba za ibada kwa
sababu kuna watu wanatumia mgongo wa misikiti kufanya maovu na kuchafua dini
yetu.”alisema Masenza
Katika hatua nyingine mkuu huyo alitumia nafasi hiyo
kutoa wito kwa wananchi kuunga mkono serikali ya awamu ya tano kwa kuwa inawaletea
maendeleo ya kweli kwenye maeneo yao.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kilolo Asiah Abdallah na Mkuu wa Wilaya ya
Mufindi Jumuhuri Willium walisema licha
ya kuwataka wananchi na waumini wa dini ya Kiislamu kutumia vyema mwezi huo
mtukufu wa ramadhani jamii
ijikite katika kuombea kazi nzuri zinayofanywa
na Rais Dk.John Magufuli.
Kwa upande wao shekhe wa Mkoa wa Iringa, Abubakari
Chalamila na wa Wilaya ya Kilolo Athuman Mnyambwa walisema mapambano aliyoyaanza rais yanalenga kutetea
rasilimali za taifa pamoja na kuwatetea wananchi
wanyonge.
Comments
Post a Comment