MBUNIFU WA CHOPA YA KUBEBA WATALII, MBIONI KUKATA TAMAA.
Peter Akaro
KILA mwanadamu kuna
mipango mikubwa ambayo angependa kuikamisha katika maisha yake hapa duniani,
ili kufanikisha hilo kujitoa sana kuna hitajika pia.
Saidi Omary ni
mbunifu kutoka Visiwani Zanzibar ambaye amepania siku za usoni kurusha angani
chopa yake ambayo ipo mbioni kukamilika.
Anafikia hatua hiyo
mara baada ya kufanikiwa kuunda magari mawili na baloni (popobawa) ambayo
haitofautiana na chopa lakini hubeba watu wasiozidi watatu, tuachane na hilo
kwanza.
Mwaka 2013 ndio
alianza kutengeneza chopa yake kama inavyoonekana pichani, lengo lake kuu ni
kuuonyesha ulimwengu uwezo na kipaji chake ili jamii na serikali kuanza kuheshimu
kazi za wabunifu.
“Hadi sasa
nimeshafunga injini yenye ‘house power’ 18 na baadhi ya vifaa vya ndani, na nje
kama mapanga boi, kilichobaki ni majarabio ya kurusha... nina uhakika itaruka
kwa ubunifu niliyouweka.
“Wala sijasomea popote
bali ni kipaji tu, na kwa vile mimi ni mbunifu katika mambo haya si kazi ngumu
kama wengi wanavyofikiri,” anasema.
Kama nilivyoeleza
awali, Omary ameunda baloni ambayo mara nyingi hutumiwa na watalii hasa katika mbuga
za wanyama, anabainisha kuwa baloni hili linatumia mafuta ya taa kama chanzo
cha nishati katika safari zake.
Kwa bahati mbaya Mamlaka
ya Anga Visiwani Zanzibar ilimueleza na kumuonya juu ya yeye kurusha baloni
hiyo kutokana hajasomea urubani wale hana utaalamu huo.
“Pia nikahangaika
hadi huko Dar es Salaam kwenye Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech) nikaja
kuomba kibali, nikafanya uwasilishaji wa wazo langu, na wakanihaidi wangekuja
kwa ajili kuutazama mradi wangu lakini hadi leo hawajafika,” anasema.
Omary, anaeleza
katika mipango yake ya baadae licha ya umri kumtupa mkono ni kutoa matoleo
tofauti tofauti ya chopa hadi kufikia 10, yaani akianzia ‘sugu air force 01’
hadi ‘Sugu air force 10’.
Hizi ni kwa ajili ya kubeba watalii na abiria wa kawaida, kuzima moto
katika ajali, ila kadiri muda unavyozidi kwenda ndoto hiyo inazidi kufifia
kutoka na kukosa masaada wa vyombo husika.
Gari alilounda Saidi Omary ambalo lilishinda tuzo kutoka Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech) mwaka 2012.
KUUNDA MAGARI.
Mwaka 2000 Omary aliunda gari ambalo alilipa jina la ‘Sugu One’ na 2006 akaunda lingine lilojulikana kama ‘Sugu Two’ ambalo 2011 alikuja nalo Dar es Salaam katika maonyesho ya miaka 50 ya Uhuru.
Anasema katika maonyesho hayo aliweza kuwa mshindi wa kwanza katika ubunifu na Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech) kumzawadia sh. milioni mbili, na kumuhaidi kumpatia fedha za kwenda kujiendeleza.
Lakini fedha za kumuwezesha ambazo zilikuwa ni zaidi ya sh. milioni 12 hazikumfikia hadi leo. Anaeleza kuwa fedha hizo zilitumwa kwa Makatibu wa Wakuu wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais.
“Nilifuatilia kwa wabunge wangu, hadi nikapiga simu Costech kwa Dkt Mshana na kumueleza hilo, lakini aliniambia hilo hawezi kuingilia kwa sababu ofisi hiyo ndio ilifanikisha mimi kwenda kwenye hayo maonyesho.
“Pia hawezi kuingilia mambo ya huku (Zanzibar) kwa sababu ya mambo ya kisiasa.... mimi nilivyoona hivyo nikaamua kuachana nao, lakini zile fedha zililetwa kwa sababu niliona katika vitabu vya bajeti na hadi leo ninavyo vitabu hivyo,” anasema.
Katika kufanya mambo yote haya, Omary elimu yake ni ya darasa la saba tu, licha ya kwenda sekondari hakuweza kuhitimu kwani aliishia kidato cha tatu ndipo akaamua kujikita katia ubunifu.
Anaeleza katika kazi yake ya ubunifu hakuna faida anayopata kwa sasa zaidi ya umaarufu na kufahamiana na watu wengi.
“Na ukiangalia gharama zote ninazotumia kuandaa hii miradi zinatoka mfukoni kwangu, hakuna anayechangia na hizo fedha ni vigumu kurudi kwa sababu ubunifu katika nchi yetu bado haujawa katika mfumo wa kibiashara,” anasema.
Omary anashauri serikali kuwainua wabunifu kwa kutunga sera ambazo zitatambua mchango wao na kuweka kazi zao katika mfumo rasmi wa kimatumizi.
COSTECH WAZUNGUMZA
Mkurugenzi Mkuu Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech), Hassani Mshinda amesema kuna wabunifu wa aina mbili, kwanza kuna wale wa Tehema ambao mara nyingi wanatengeneza ‘soft ware’ na hawa wamekuwa wakifanikiwa sana sokoni kwa sasa.
Na kuna wabunifu ambao ni ‘wakitamaduni’, wanachokifanya ni kutengeneza kitu ambacho tayari kipo ila kwa namna nyingine, ubunifu huu si rahisi sana kwenda sokoni.
Msinda anasema gari alilotengeneza Omary, hadi kuanza kutembea barabarani na kupata vibali vya kiusalama ni mchakato mrefu, na pia gari hilo hatoweza kulitengeneza kwa kiwango kile kinachohitajika.
“Huyu kazi yake ni fundi seremala, hili gari amelitengeneza kiutundu tu, tulipomuuliza tumsaidi vipi hakuwa na hamasa sana kwa sababu alijua kazi hii haiwezi kumletea fedha wengi tunawashauri watengeneze vitu ambavyo vinaleta faida kiuchumi na kijamii.
“Lakini wale ambao wanaweza kuendelea wanaweza kufanya hivyo, ila hatuwezi kuwapa fedha za umma kwa kufanya kitu ambacho tayari kipo, isipokuwa tunajaribu kuwapatia vifaa ili kuendelea,” anasema Msinda.
Anashauri watu wajikite kwenye ubunifu ambao una maanufaa katika jamii, kwa mfano wanaobuni mashine kwa ajili ya kilimo na uzalishaji umeme wamekuwa wanafanya vizuri na wamekuwa wanawaunga mkono.
Mshinda anasema ubunifu wa aina hii wamekuwa wakiuunga mkono kwani wanaamini utafanikiwa na hata ukiingia sokoni utaweza kuleta ushindani.
“Zamani ulikuwa unafanya ubunifu na kuuendeleza kisha unapeleka sokoni, ila sasa unapofanya ubunifu unaangalia kitu gani kinahitaji katika jamii, kisha unaenda kukitengeneza, hao ndio wanandelea vizuri,” anasema.
Anasema wakina Omary ni watu watundu tu ambao wameamua kutumia tu vipaji vyao, kwa mfano mtu anakueleza ametengeza gari lakini ukiangalia hakuna kitu kipya alichokiweka.
“Mara nyingi wanakuwa ni watundu na sio wabunifu haswa, kwa mfano yule kijana ambaye yuko Mbeya ambaye watu walikuwa wanasema ametengeneza chopa, tulienda kuiangalia na ili chopa haikuwahi kuruka lakini vyombo vya habari mlipamba sana,” anasema.
Licha ya Adam kutengeneza chopa alikuwa hajawahi kuiona, hivyo kilichofanyika ni kumpeleka kwenda kuiona ambapo kuna sehemu ndege ilikuwa imeanguka ikawa inafanyiwa matengenezo hivyo akapata fursa ya kuona kinachofanyika.
Pia alipelekwa jeshini kushuhudia chopa ilivyo na namna inavyofanya kazi.
“Alipongia ndani alijua vitu vingi na kugundua kuwa anaweza kufanya vitu vingine vya maana kuliko chopa ambayo hana uhakikika kama itaruka.
“Kweli alipata hamasa ya kwenda kutengeneza vitu vingine, sio chopa tena, na sasa tunaangalia namna ya kumasaidia vifaa kwa sababu ana vijana zaidi ya 14 ambao wanajifunza kwake, yeye ni fundi magari pia hivyo anaweza kutengeza ajira,” anasema Mshinda.
Saidi Omary akiwa karibu na chopa anayoiunda kwa sasa.
Comments
Post a Comment