MIKOA YA IRINGA NA NJOMBE WATOTO WANAPATWA NA UTAPIAMLO NA KUDUMAA KWA KUKOSA LISHE.
Na Mwandishi Wetu,
Iringa.
IMEELEZWA kwamba
watoto wengi nchini wanapatwa na tatizo la utapiamlo pamoja na kudumaa kwa
sababu ya kukosa lishe bora kutokana na wazazi kutokuwa na uelewa kuhusu lishe
bora kwenye familia zao.
Aidha Mikoa ya Iringa
na Njombe ni mikoa inayolima mazao ya chakula kwa wingi ikiwamo viazi, uwele,
ngao pamoja viazi vitamu lakini licha ya kuwa na sifa hizo za uzalishaji bado
wazazi hawana elimu ya kuwapatia watoto wao lishe bora.
Wito huo umetolewa na
Umoja wa Wanafunzi wa Chuo Kikuu Kikatoliki cha (RUCU), wanaosomea sayansi ya
afya na mazingira (REHSA).
Wakizungumza na wazazi
na walezi jana kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa baadhi ya wanafunzi wa
Chuo hicho Wajabu Abdulrahaman na Fadhili Katula walisema kuwa wao kama
wanafunzi wameandaa mafunzo kwa lengo la kutoa elimu ya lishe kwa kina mama
wanaolea na wajawazito.
Hata hivyo walisema mafunzo hayo yatalenga pia wazazi wenye watoto waliochini ya umri wa miaka mitano ili waweze kupambana na
tatizo la udumavu na maradhi.
Wanafunzi
hao walisema baada ya kutoa elimu hiyo, wanatarajia kuona jamii ya
Iringa ikizingatia lishe bora huku wakizungumzia changamoto mbalimbali
wanazokumbana nazo wakati wa utoaji elimu hiyo kwa jamii.
Walisema moja ya
changamoto wanazokumbana nazo ni uelewa mdogo kutoka kwenye jamii juu ya lishe
bora, hawajui ni vyakula gani vinapatikana kwenye maeneo yao ambayo yanawasaidia akina mama wajawazito pamoja na watoto wao.
Ofisa Lishe
Hospitali ya Mkoa wa Iringa, Neema Mtekwa , alisema muitikio wa jamii juu
ya lishe ni hafifu hususani kwa kina baba hali iliyosababisha kushindwa kufikia
lengo la kutokomeza udumavu kwa watoto.
REHSA ni umoja wa
wanafunzi wanaosoma Sayansi ya Afya na Mazingira katika Chuo Kikuu cha Rucu
ambao wamekuwa wakizunguka katika kata mbalimbali za Mkoa huo kwa lengo la
kutoa elimu kwa jamii ili kuondokana na tatizo la udumavu na utapiamlo
kwa watoto mkoani Iringa.
Comments
Post a Comment