SERIKALI HAITACHUKUA HATUA KWA CHOMBO CHA HABARI KINACHOKOSOA.
SERIKALI imesema kuwa hakuna chombo chochote cha habari kitakachochukuliwa hatua kwa kuandika habari zenye mrengo wa kukosa sera na utekelezaji wake kama ambavyo wadau wengi wamekuwa wakiaminisha umma.
Kauli hiyo imetolewa leo na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo Dkt. Hassan Abbasi wakati akizungumza katika Kipindi cha Habari Kuu kinachorushwa na Kituo cha Televisheni cha Startv mjini Dodoma.
Dkt. Abbasi amesema kuwa Sheria na 12 ya Huduma za Habari ya Mwaka 2016 kifungu cha 51 kinatoa ruhusa kwa chombo cha habari kukosoa kwa lengo la kuonyesha njia mbadala katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.
“Hakuna chombo cha habari kitakachochukuliwa hatua kwa kukosoa, haki hiyo ipo kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Habari ya Mwaka 2016 kifungu cha 51, tutaendelea kuthamini na kufanyia kazi ukosoaji huo,” alisema Dkt. Abbasi.Hata hivyo Dkt. Abbasi amesisitiza kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua kwa chombo kitakachokiuka sheria na misingi ya maadili ya taaluma ya habari kwa lengo la kulinda maslahi ya taifa.
Dkt. Amesisitiza kuwa ni vyema wamiliki wa vyombo vya habari wakatumia uhuru huo wa kisheria kuchapisha habari zenye nia njema kwa mustakabali wa maendeleo ya nchi badala ya kueneza hofu miongoni ya mwa jamii.
Akijibu swali la muongozaji wa Kipindi kuhusu kufungiwa kwa Gazeti la Mawio, Dkt. Abbasi amesema kuwa Gazeti hilo halijafungiwa kutokana na kuandika habari ya kukosoa Serikali isipokuwa limekiuka miiko ya taaluma kwa kuandika habari za kushushia heshima na hadhi ya mtu katika jamii pamoja na kukiuka maagizo halali ya Serikali.
Alisema kuwa kama ingekuwa kulifungia Gazeti hilo kwa sababu ya kuandika habari za kukosoa pengine lingekuwa limefungiwa muda mrefu kutokana na ukweli kwamba Gazeti hilo mrengo wake unafahamika kuwa ni wa ukosoaji.
Akizungumzia dhana ya uhuru wa habari, Dkt. Abbasi amesema kuwa ipo haja ya wadau wa habari kufahamu dhana halisi ya uhuru wa habari badala ya kuendelea kufanya makosa ya tafsiri isiyo sahihi jambo ambalo linapotosha dhana nzima ya uhuru wa habari.
Dkt. Abbasi amesema kuwa Mkataba wa Kimataifa wa mwaka 1966 wa Haki za Kiraia na Kisiasa, ibara ya 19 inaeleza haki za kupata habari ambayo inaenda sambamba na ukomo wa kutoa taarifa kwa maslahi ya nchi.
Aidha Dkt. Abbasi ametoa rai kwa wadau wa habari nchini kuisoma sheria ya huduma za habari ya mwaka 2016 iliyoanza kutumika rasmi badala ya kuyaachia makundi ya wanaharakati wapotoshe uhalisia wake.
Akizungumzia utekelezaji wa Sheria hiyo, Dkt. Abbasi amesema kuwa sheria imekwishaanza kutekelezwa katika hatua kadha ambapo alizitaja baadhi ya hatua hizo kuwa ni pamoja na utoaji wa Vitambulisho vya Waandishi wa HabarI.Alisema kuwa utoaji wa Vitambulisho hivyo umelenga kuwajengea uwezo wa kujiendeleza waandishi wa habari katika kipindi cha mpito cha miaka mitano ili kufikia vigezo stahiki vya taaluma.
Tanzania imeingia katika Historia baada ya kutunga Sheria na 12 ya Huduma za Habari ya Mwaka 2016 ambayo imefuta Sheria ya Magazeti ya Mwaka 1976 ambayo imepitwa na wakati kutokana na mabadiliko ya teknolojia, uchumi na utamaduni.
Comments
Post a Comment