BELENG’ANYI, MBUNIFU MWENYE MALENGO YA KUTENGENEZA MGODI WA KUFUA UMEME.
Peter Akaro
BINADAMU anazaliwa na
ubunifu au mazingira anayokuliwa yanaweza kumfanya kuwa hivyo.
Makala ya leo yatazungumzia
maisha ya mbunifu Ntibanga Beleng’anyi ambaye anatengeneza mashine za kukamulia
juisi ya miwa na kuunda magari.
Pengine vitu hivi si
vigeni katika mazingira yetu, ila kilichopelekea makala haya kuandikwa, ni
namna Beleng’anyi alivyoweza kutengeneza vitu hivi bila kusomea sehemu yoyote.
Ndiyo hakusoma, Baada ya
kumaliza Shule ya Msingi Ng’wang’iwita iliyopo Bariadi Shinyanga, mwaka 2005 aliamua
kuja Dar es Salaam kwa ajili ya kazi za kibunifu kwa sababu upatinaji wa vifaa
ni rahisi, vitu alivyofanikiwa kutengeneza ni kama.
Hii ni mashine ya kutengenezea juisi ambayo inatembea umbali wa kilo mita 400.
MASHINE YA JUISI.
Mashine ya kukamua juisi
ya miwa ambayo kaitengeneza yeye ina utofauti katika vitu viwili ukilinganisha
ni zile zilizozoeleka, kwanza mtumiaji ana uwezo wa kuitembeza hadi umbali wa
meta 400 kutokana ina matairi.
Pili mashine inapokuwa
inafanya kazi inaweza kuzalisha umeme wake kwa ajili taa na hata redio, hapa ni
pale injini inapokuwa inafanya kazi na hata itakapozimwa umeme uliozalishwa
unahifadhiwa.
Pia matumizi yake ya
mafuta si makubwa sana, kwani lita mbili zinaweza kutumia ndani ya masaa sita
ila inatengemea na matumizi ya muhusika.
“Tokea mwaka jana
ninatengeneza hizi mashine, gharama zinatofautiana kulingana na upatikanaji wa
vifaa, kwa hiyo bei inaweza kuwa kati ya sh. milioni mbili hadi tatu,” anasema.
Anaeleza kuwa alianza kazi
ya kutengeneza hizi mashine kutoka na kupenda kuwa mjasiriamali katika ufundi
stadi ili kuweza kujikwamua kimaisha.
“Unapoona kazi inatendeka
kwa kiasi fulani inabidi mbunifu uindeleze zaidi ili kuleta matokeo bora zaidi,”
anasema Beleng’anyi.
KUUNDA MAGARI.
“Niliamua kuanza kuunda magari kwa sababu
hakuna sehemu ya kwenda kuajiriwa na pia sijapita katika mfumo wa kuweza
kutambulika,” anasema
Gari alilounda mwaka 2012 lilikuwa
linatumia mafuta lita moja kwa kwenda umbali wa kilometa 18 hadi 20, na
lilikuwa linaenda kwa spidi 50 hadi 80 kwa saa moja ila ilitengemea na aina ya
barabara pia.
“Niliachana na mpango wa
kuunda magari kutokana na kusumbuliwa barabarani na polisi, waliniuliza kwa
nini umetengeneza kitu ambacho hakina usajili wala kadi, pili walikuwa wakisema
huu ni mtambo na si gari, nilipoona usumbufu umezidi ndipo nikalipeleka
kijijini kwetu.
“Zilikuwa ni ndoto zangu
tangu nikiwa nasoma nilisema siku moja nitaunda gari, kama ningepata shule ya
moja kwa moja ningekuwa mbali sana, na hivi vyote ninavofanya sasa si kwamba
vimeibuka tu kipindi hiki bali ni ndoto za muda mrefu,” anasema na kuongeza.
“Nilijaribu kwenda kufanya
usajili wa gari wakanieleza nipeleke nyaraka zitazoonyesha gari limenunuliwa
nchi gani, limetembea umbali gani, niliposhindwa hayo nikalipelekea kijijini
kama nilivyoeleza awali,” anasema.
Anaeleza kwa sasa gari
kijijini linatumika kwa kubeba maji na mizigo mbali mbali yenye uzito wa hadi
kufikia tani moja.
“Gari hili linafaa kwa
matumizi ya kijijini kwa sababu licha ya kukusafirisha, linaweza kuvuta maji
kwenye kisima, na pia ukafunga kinu kwa ajili kukoboa mahindi au mpunga,”
anasema.
Hili ni gari ambalo aliliunda ila kutokana na usumbufu aliokuwa akiupata barabarani aliamua kurudisha kijijini.
WALIOSOMEA FANI WANAFANYA NINI.
Pengine waliopita katika
mfumo rasimi, yaani shule muda mwingine wanaweza wasiweze kufanya kama yeye, je
nini kinapelekea hali hiyo?
Anajibu kwa kusema wengi
(wanafunzi) wanakwama kwa sababu wanachofundishwa mara nyingi ni tofauti na
kile ambacho wanatakiwa wakifanye kwa vitendo.
“Kuna vitu vinakuwa vinakinzana,
siku zote ubunifu huwa ni wa mtu, hakuna shule ambayo utafundishwa hilo au kufikiria,
shule unafundishwa tu zile kanuni za msingi, lakini katika muendelezo wa maisha
hautakiwi kukariri bali kuwa mbunifu,” anasema Beleng’anyi.
Anaeleza kuwa licha ya
wabunifu wengi kuonyesha uwezo mkubwa hakuna jitihada za makusudi zinazofanyika
ili kuwainua.
“Hata nilipotengeneza lile
gari nilienda Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech) wakaniambia sawa umetengeneza
gari, lakini umetumia vifaa vya watu wengine inabidi ni tengeneze vyangu.
“Hii dunia ina kila kitu,
kinachotakiwa ni wewe kuvikusanya na kuunda unachotaka, sasa ukianza kila kitu utengeneza
wewe utakuwa ndio umeanza mwanzo, na gharama zitakuwa kubwa,” anasema.
MALENGO
YA BAADAYE.
Beleng’anyi anasema malengo
yake si kuendelea kutengeneza vitu vidogo vidogo kama hivi, bali ni kutengeneza
‘mgodi’ wa kufua umeme na tayari ameshafanya utafiti na kugundua anaweza kuzalisha
kwanzia KV 30 hadi Megawatts 10 za umeme.
“Sasa hivi serikali
imekuwa na mkakati wa kupeleka umeme vijijini, ila mimi nitakuja na mkakati wa
kupeleka umeme mashambani.
“Ina maana tuchimbe visima
kwa ajili ya umwagiliaji na ufugaji, hii itakuwa na faidi kuliko kupeleka umeme
kijijini kwa ajili ya kuwasha taa tu, hiyo haiwezi kumletea mwananchi maendeleo
bila kuwa na shughuli za kiuzalishaji,” anasema na kuongeza.
“Itawezekana kwa sababu
tupo katika mabadiliko ya ukuaji wa viwanda, tunatakiwa tushindane katika hoja
za kitenolojia na si vingonevyo, cha msingi serikali ituangalie,” anasema
Beleng’anyi.
Comments
Post a Comment