BARAZA LA MADIWANI LAUTAKA UONGOZI WA WILAYA IRINGA KUTEKETEZA ZANA ZA UVUVI HARAMU.
Na Mwandishi Wetu. Iringa.
BAADHI ya
Madiwani wa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Iringa vijijini, limeutaka
uongozi wa Wilaya ya Iringa kuteketeza zana haramu za uvuvi zilizokamatwa
kwenye msako wa kukamata zana haramu za uvuvi katika bwawa la Mtera kwakuwa
zana hizo zimegeuzwa biashara na baadhi ya watendaji ambao wanaohifadhi
zana hizo.
Madiwani hao waliyasema hayo
mwishoni mwa wiki kwenye kikao cha baraza hilo ambapo baadhi ya
madiwani wamehoji uhalali wa samaki wadogo kuendelea kuuzwa katika baadhi ya
masoko mkoani hapa likiwamo soko kuu la mjini Iringa huku mamlaka zinazohusika
zikiendelea kulifumbia macho jambo hilo.
Nao baadhi ya madiwani wa
halmashauri hiyo akiwamo Diwani wa Kata ya Migori, Majaliwa Lyaki
alisema kuwa”Kuna watu wanapiga dili na kuna siku moja nilikuwa nashuhudia kati
ya wale waliopo kwenye kikosi kazi amesema aliitangaziwa donge nono la
sh.300,000 ili kokora lake lipate kuondoka ni kwasababu tu nyavu zimekaa muda
mrefu pale,na mara nyingi tumekuwa tukifanya mawasiliano na wataalamu hakuna
lolote zaidi ya kusema tu kwamba Mkuu wa Wilaya atakuja kuyachoma na hatujui
anakuja kuchoma lini.”alisema Lyaki.
Diwani wa Kata ya Lowa,
Charles Nyagawa, alitaka kujua kwa mfano mtu akikamatwa na pembe za ndovu
zikisafirishwa kwenda Dar es salaam hawasemi mamlaka tofauti wanamkata sasa leo
samaki wadogo wanauzwa sokoni na kutaka kujua hilo suala la samaki ni suala la
kitaifa au nisuala la halmashauri?
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Iringa, Abel Mgimwa, alisema
Halmashauri yake itazingatia ushauri wa Baraza la Madiwani kukomesha uuzwaji wa
samaki wachanga hasa katika soko kuu la mjini Iringa ili kuhakikisha wavuvi na
wafanyabiashara wanapenya na kutorosha samaki hao wachanga wanadhibitiwa hadi
sokoni.
“Sisi kama Halmashauri
tutawasiliana na mamlaka stahiki za hilo soko mamlaka zote zinazohusika na hilo
soko kuwahakikishia kwamba hawatakiwi kuuza hao samaki wadogo pale hivyo
ushauri tumeupokea tukishakutana nao tutawaeleza na wao waeleze kuchukua hatua
stahiki dhidi ya samaki hao.”alisema Mgimwa.
Halmashauri ya Iringa
Vijijini kwa kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Iringa
imekuwa ikiendesha msako wa kukamata zana haramu za uvuvi pamoja na samaki
wachanga wanaovuliwa kinyume cha sheria.
Hata hivyo zoezi hilo limeonesha kutofanikiwa kwa kiasi
kikubwa kutokana na baadhi ya Halmashauri zinasimamia baadhi ya maeneo ya bwawa
la Mtera ikiwamo Mpwawa na Chamwino kushindwa kuendesha zoezi kama hilo .
Comments
Post a Comment