BALOZI SEIF, SERIKALI YAKE INASUBIRI MAPENDEKEZO YA RASIMU YA SERA YA HABARI.
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar.
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi
Seif Ali Iddi amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inasubiri kuyapokea mapendekezo
yatakayowasilishwa ya Rasimu ya Sera ya Habari Zanzibar ili kuyafanyia
kazi ili aone Sekta ya Habari Nchini inakuwa imara.
Aidha Taasisi
zinazohusika na jukumu la kusimamia masuala hayo ni vyema zikahakikisha
kwamba zinaharakisha mapendekezo hayo ili ile dhana ya Uhuru wa kupata Habari
bila ya kuogopa inapatikana.
Katika taarifa iliyotumwa
kwenye vyombo vya habari leo na Ofisi ya
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Othman Khamis Ame, inasema leo , Balozi
Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati wa mazungumzo yake na Uongozi wa Baraza
la Habari Tanzania (MCT) ulioongozwa na Katibu Mtendaji Kajubi Mukajanga aliokutana nao Ofisini kwake
Mtaa wa Vuga Mjini Zanzibar.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar imeahidi kutoa kila aina ya msaada katika kuona Sekta hiyo muhimu kwa
jamii inawajibika ipasavyo katika kuwapasha habari wananchi.
“Habari ni Sekta
muhimu inayotoa Taarifa na Elimu na kuwahusisha moja kwa moja wananchi wa
kawaida wakiwemo wakulima vijijini ”. alisema Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar.
Pia Balozi Seif kupitia
Uongozi wa MCT aliwakumbusha wanahabari kuzingatia sheria na maadili ya kazi
katika kuandika habari wanazozifanyia utafiti wa kina ili zisaidie wananchi
kupata habari za ukweli.
Alisema changamoto ya Vitambulisho vya
Kazi inayowakumba wana habari wanaotokea Tanzania Bara na kupangiwa kufanya
kazi Zanzibar Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliahidi kulifuatilia kwa kina
suala hilo ambalo bado halijawa kero kama yalivyo masuala mengine katika
utendaji.
“Waandishi wa Habari wanaotokea Tanzania
Bara wanapaswa kuandaliwa utaratibu maalum wa kupata vibali vya kazi kwa vile
wao hawahusiani na kuwa na Vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi
katika kuomba kibali cha kufanya Kazi Zanzibar,”alisema
Alieleza kuwa mfumo unaotumika
katika kuwapasha habari wananchi wa pande zote za Muungano hauna mipaka
licha ya kwamba Sekta ya Habari sio Taasisi iliyomo ndani ya masuala ya
Muungano.
Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar aliupongeza Uongozi ( MCT) kwa umakini wao wa kusimamia Sekta ya
Habari Nchini.
Naye Katibu Mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga alisema Kamati ya Maadili ya
baraza hilo imekuwa na utaratibu wa kufanya ziara za kusikiliza
malalamiko yanayotolewa na wananchi wanaoandikwa visivyostahiki katika vyombo
mbali mbali vya Habari.
Alisema Wajumbe wa Kamati hiyo kupitia
ziara hizo hupata fursa za kushauri, kuelekeza pamoja na kuwaonya na wengine kuwachukuliwa
hatua za kisheria wana habari wanaofanya makosa katika kuandika habari
chafu dhidi ya wananchi.
Naye Mkuu wa MCT upande wa Zanzibar, Shifaa Hassan, alisema Mchakato wa Sera ya
Habari Zanzibar umeanza tokea mwaka 2010 kwa mashirikiano baina ya Idara
ya Habari Maelezo, Tume ya Utangazaji Zanzibar pamoja na baadhi ya Viongozi wa
Taasisi za Serikali.
Shifaa alisema Zanzibar imekuwa tajiri
katika masuala ya Historia ya Habari kutokana na kuanza mapema kwa Sekta hiyo
ndani ya Ukanda mzima wa Afrika ya Mashariki.
Alisema Ofisi ya Baraza la Habari
Tanzania upande wa Zanzibar ilianzishwa mwaka 2003 na kuanza na Mpango
Maalum wa harakati za kutoa mafunzo kwa Wana Habari wachanga wa
vyombo mbali mbali vya Habari wakiwemo pia wale waliomaliza masomo yao ya
sekondari walioamua kujiunga na Tasnia hiyo.
Katibu
Mtendaji wa Baraza la Habari Bwana Kajubi Mukajanga akimkabidhi Balozi
Seif Vitabu mbali mbali vilivyochapishwa na Baraza hilo kuhusu Tasnia ya
Habari Tanzania.
Balozi Seif akiwa katika picha ya pamoja na Uongozi
wa juu wa Baraza la Habari Tanzania mara baada ya kubadilishana mawazo Ofisini
kwake Vuga Mjini Zanzibar, Kushoto ya Balozi Seif ni Katibu Mtendaji wa Baraza
la Habari, Kajubi Mukajanga na Muandishi wa Makala wa MCT Yussuf
Mpinga.
Katibu Mtendaji wa Baraza
la Habari (MCT) Kajubi Mukajanga Kulia ya Balozi Seif akielezea mikakati ya
Baraza la Habari Tanzania inavyofanya kazi Zanzibar katika kuhakikisha Maadili
ya Habari yanazingatiwa na wanahabari wote Nchini.
Makamu wa Pili wa Rais
wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Uongozi wa Baraza la Habari
Tanzania MCT uliofika Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar kubadilishana nao
mawazo.
Comments
Post a Comment