WA-SHIA WAFADHILI MATIBABU YA WATOTO 40 WENYE TATIZO LA KICHWA KIKUBWA.


Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Azim Dewji akizungumza na baadhi ya wafanyakazi wa MOI na waandishi wa habari (hawapo pichani) mapema leo, (mwenye koti jeupe) ni Mkurugenzi wa Tiba wa taasisi hiyo, Dk. Samwel Swai.

Na Veronica Romwald, Dar es Salaam

WAUMINI wa dhehebu la Shia nchini wamejitolea kuwezesha matibabu ya watoto 40 waliozaliwa na tatizo la kichwa kikubwa ambao wamelazwa katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI).

Akizungumza na waandishi wa habari mapema leo, Mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Azim Dewji amesema matibabu hayo yatagharimu kiasi cha Sh. milioni sita.

Mkurugenzi wa Tiba wa MOI, Dk. Swai akiwafafanulia jambo wageni hao.

“Wiki mbili zilizopita tulikuja MOI na tukajitolea uniti 140 za damu lengo ni kufanikisha upasuaji wa watoto hawa na tulikusanya fedha kwa ajili ya kuwezesha matibabu yao.

“Leo tumekuja tena, tumeahidi kuendelea kuchangia damu kupitia shule ya Al-Muntazil. Wananchi wajue kwamba madaktari hawa wanafanya kazi kwa moyo na kwa kujitolea ili kuokoa maisha ya ndugu zetu hawa, ombi langu kwao waje wajitolee damu.

Hapa wakiwa wodini

“Wamenidokeza kila wiki zinahitajika uniti 100 kufanikisha upasuaji, sasa Mungu ametujalia afya nzuri hivyo ni vema nasi tujitolee kusaidia wengine,” ametoa rai.

Amesisitiza “Ukitoa damu hutakufa, jinsi tulivyoumbwa na Mungu ndani ya miezi mitatu hadi minne damu yote uliyotoa inakuwa imerudi, ukitoa damu unapata faida kuu tatu, kwanza unakuwa mtu mwenye huruma, unapata thawabu kwa Mungu na unakuwa umeokoa maisha ya mtu.

Amesema jumuiya hiyo imejiwekea utamaduni wa muda mrefu kuchangia damu katika Mpango wa Taifa wa Damu Salama kila mwaka angalau mara moja lakini sasa wanakusudia kuchangia mara nne hadi tano.

“Tulikuwa tunafanya hivyo kila inapofika mwezi wa Ramadhani sasa tutajitolea si mara moja tu kwa mwaka bali nne hadi tano hivyo nawaalika na waumini wa wananchi wengine tuungane kuchangia damu,” amesema.

MOI KUTOA ELIMU JINSI YA KUMUEPUSHA MTOTO NA TATIZO LA KICHWA KIKUBWA NCHI NZIMA



https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEhO3TJ44iv4zCR21C3BJ3oftQwRam62ds7hW5un5Ml9UNVXmzyRTnj8N3p8guljm-VKF5lXffWADuB8Io0zRXIplRESiAU4NMKYIOFRR23oC_-dmmQHRz0vRo4OQWtfbC8biodFyR7Wm9Ti/s1600/9.jpgNa Veronica Romwald, Dar es Salaam

TAASISI ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI) inatarajia kufanya kampeni maalumu ndani ya mwaka huu ya kuhamasisha jamii kutambua jinsi ya kuepuka mama kuzaa mtoto mwenye tatizo la kichwa kikubwa na mgongo wazi.

Mkurugenzi wa Tiba wa MOI, Dk. Samwel Swai ameeleza hayo mapema leo alipozungumza na waandishi wa habari walipotembelewa na viongozi wa dhehebu la Shia ambao wameahidi kusaidia matibabu ya watoto 40 yaatakayogharimu Sh milioni sita.

“Tatizo hili lipo kwa muda mrefu sasa nchini, leo idadi imeongezeka kwa sababu jamii imepata uelewa, tunajitahidi kuwatibu kwa kadri ya uwezo wetu, tiba yao ni mtambuka na ina vitu vingi mno kuikamilisha, tunahitaji damu ya kutosha, usafiri wa kuwatoa huko walipo, dawa za usingizi na vifaa vya kutosha ili kuwahudumia,” amesema.

Dk. Swai (anayezungumza) amesema wamejitayarisha kuwasaidia wale waliowaandaa huku lengo lao kwa sasa ikiwa ni kutoa elimu kwa wananchi.

“Ni tatizo linaweza kuzuilika kwa kutumia lishe (folic acid) ambayo hupatikana kwenye baadhi ya vyakula lakini tunatoa vidonge maalumu vya folic acid, mama anatakiwa ameze miezi mitatu kabla ya kubeba ujauzito,” amesema.

Amesema pia wamekusudia kupata wodi maalumu na wataalamu watakaoshughulika kuwasaidia watoto hao peke yao.

“Tukihamia rasmi huku jengo jipya kule kwenye jengo la zamani tutaweka chumba kimoja cha upasuaji maalumu kwa ajili ya watoto hawa peke yao,” ameweka wazi.

Amesema jumamosi hii wanatarajia kuwafanyia upasuaji kati ya watoto 25 hadi 30 ambao tayari wameandaliwa.

Jumatano, 19 Aprili 2017

TAASISI YA MOYO YA JAKAYA KIKWETE TEGEMEO AFRIKA MASHARIKI



Na Veronica Romwald, Dar es Salaam

Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Profesa Mohamed Janabi amesema kwa sasa taasisi hiyo inategemewa na nchi zote zilizopo Afrika Mashariki katika kutoa matibabu ya moyo hasa kwa watoto. 

Profesa Janabi amesema hayo leo alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu huduma ya upimaji wa kugundua magonjwa ya moyo mapema kwa mtoto aliyeko tumboni mwa mama yake.  
"Tunafanya vizuri sasa katika ukanda wa Afrika mashariki, tunategemewa hasa katika oparesheni za magonjwa ya moyo kwa watoto," amesema.

Amesema hadi sasa wameshawatibu watoto kutoa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Komoro na Kenya.

"Tupo madaktari wa moyo 15, kati yetu watatu ni wa watoto, ili kuongeza idadi hiyo kuna weznetu wapo masomoni nchini Afrika Kusini na Israel hivi sasa," amesema.

Ameongeza "Changamoto kubwa tuliyonayo ni nafasi, tunahitaji jengo lingine, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ameahidi kutupatia.

"Nia yetu tuwe na jengo maalumu kabisa kwa ajili ya watoto, hiyo itatupa fursa ya kufanyavitu vingi zaidi kuliko ilivyo sasa," amesema.

JKCI YAPIMA MOYO WA MTOTO ALIYE TUMBONI MWA MAMA YAKE


Dk. Naiz akionesha jinsi wanavyofanya upimaji kuchunguza magonjwa ya moyo wa mtoto aliyeko tumboni. 

Na Veronica Romwald, Dar es Salaam

TAASISI ya Tiba ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kwa mara nyingine tena imefanya upimaji wa moyo wa mtoto aliye tumboni mwa mama yake, kuchunguza magonjwa mbalimbali ya moyo.

Upimaji huo umefanywa leo katika taasisi hiyo na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa Watoto wa JKCI, Naiz Majani.

Akizungumza na waandishi wa habari, Dk. Naiz amesema kuna faida lukuki iwapo mjamzito ataamua kufanya kipimo maalumu.

"Tunatumia Ultra sound kama kawaida kufanya kipimo hiki, lakini inakuwa ina tofauti kidogo... hatutumii mionzi yoyote, hivyo hakuna madhara anayoweza kuyapata mama au mtoto wake aliye tumboni," amesema. 

Ametaja faida hizo kuwa ni kupunguza idadi ya vifo vya watoto wanaozaliwa na magonjwa ya moyo, na kuwaondoa kwenye masumbufu wanayoweza kuyapata kutokana na kuchelewa kupata matibabu.

"Kwa mara ya  kwanza tuliwafanyia kipimo hicho wajawazito 25 mwishoni mwa mwaka jana ambapo watano kati yao mimba zao zilikutwa na matatizo.

"Wajawazito hao wanatarajiwa kujifungua wakati wowote kuanzia sasa na watoto hao wataanza kufuatiliwa kwa ukaribu na kupewa matibabu ya haraka," amesema.

Amesema waliamua kuanza kufanya kipimo hicho baada ya kugundua watoto kadhaa hufikishwa katika taasisi hiyo wakiwa katika hatua mbaya kiasi cha wao kushindwa kuwapatia matibabu.

Amesema inakadiriwa katika kila watoto 100 wanaozaliwa nchini mmoja anakuwa amezaliwa na magonjwa ya moyo.

"Mwaka jana inakadiriwa walizaliwa watoto milioni moja, kwa msingi huo watoto wapatao 12,000 walizaliwa na magonjwa haya lakini tuliowaona kliniki yetu ni kati ya 700 hadi 750 pekee," amesema.

"Kuna baadhi ya magonjwa ya moyo yanatakiwa kutibiwa mapema, lakini wanakuja umri umeshakwenda tunashindwa kuwasaidia," amesema.
 http://www.mwananchi.co.tz/image/view/-/3401124/medRes/1305356/-/11tcbm6z/-/pichamoyo.jpg
Amesema kwa kufanya kipimo hicho wana uwezo wa kuona asilimia 90 ya magonjwa ya moyo.

"Kwa asilimia 10 tu hatuwezi kuona, tatizo kubwa kwa watoto ni matundu. Mtoto akiwa tumboni mwa mama yake kuna baadhi ya moyo wake huwa na baadhi ya matundu ambayo hata hivyo pindi anapozaliwa yanapaswa kuzibika.

"Sasa kama tukiona hali hiyo na akazaliwa yakawa bado yanaonekana moja kwa moja tunajua hilo ni tatizo," amesema.

Amesema wanaweza pia kuona iwapo milango ya moyo wa mtoto ina tatizo au la.

"Kipindi mwafaka kwa ajili ya kufanya kipimo hiki ni pale mimba inapokuwa na wiki 18 hadi 22, kwa nchi za wenzetu wamepiga hatua zaidi, kwa sasa wapo kwenye majaribio wakigundua mtoto ana tatizo wanalitibu mara moja akiwa huko huko tumboni," amesema. 

Mkurugenzi wa JKCI, Profesa Mohamed Janabi amesema dhumuni kubwa la kuanzisha huduma hiyo ni kugundua matatizo hayo mapema.

"Tunahamasisha kina mama wajitokeze, Tanzania sasa imepiga hatua kubwa, tunafanya hivi kwa sababu asilimia 85 ya wagonjwa tunaowafanyia upasuaji ni watoto.

"Na hawa ndiyo tunaowategemea kuwa Taifa la kesho, tusipowagundua na kuwatibu mapema maana yake ni kwamba watakuja kuwa mzigo kwa Taifa miaka ijayo," amesema.

Amefafanua kwamba miaka ya nyuma si  kwamba magonjwa ya moyo hayakuwapata watoto bali hayakuweza kugundulika kutokana na uhaba wa wataalamu, vifaa. 

"Watoto wengi walikufa kwa kile kilichoelezwa ama ni typhoid, nimonia au surua, leo hii wataalamu tupo, tulikwenda kujifunza kwa wenzetu katika nchi zilizoendelea ili tuisaidie nchi yetu, magonjwa yote ya moyo yanatibika," amesisitiza.

'NEEMA YAWAANGUKIA' MADAKTARI WA TZ WALIOOMBA KUAJIRIWA KENYA

http://ghradio1.com/uploads/news/Doctors_suit4.jpgNa Veronica Romwald, Dar es Salaam

Hapana shaka yoyote kwamba madaktari wa Tanzania 258 waliojitokeza kuomba ajira nchini Kenya watakuwa wamejawa na furaha kubwa ndani ya mioyo yao hivi sasa.

Hiyo ni baada ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu kutangaza kwamba Rais John Magufuli ameamua madaktari hao wote kuajiriwa nchini mara moja, hivyo hawatakwenda tena Kenya.

Waziri Ummy amesema hayo leo mjini Dodoma alipozungumza na waandishi wa habari na taarifa yake hiyo kutumwa kwa vyombo vya habari.

"Kufuatia uamuzi huu, Majina ya Madaktari husika na vituo watakavyopangiwa kazi yatatangazwa katika tovuti ya Wizarawww.moh.go.tz pamoja na wataalamu wengine wa Afya 11 walioleta maombi yao na kukidhi vigezo.
 http://fullshangweblog.com/home/wp-content/uploads/2017/01/TUTA-2.jpg
"Aidha, Serikali ya Tanzania itakuwa tayari kushughulikia upya ombi la Serikali ya Kenya kupatiwa Madaktari 500, pale ambapo hakutakuwa na vikwazo vya kupeleka Madaktari wetu nchini Kenya," amesema.

Awali Waziri Ummy katika taarifa yake hiyo alieleza mnamo Machi 18, mwaka huu ujumbe wa Serikali ya Kenya ukiongozwa na Waziri wa Afya Dk. Cleopa Mailu uliwasili nchini ambapo ulikutana na Rais Magufuli, kwa madhumuni ya kuomba kuajiri kwa Mkataba Madaktari wa Tanzania mia tano (500) ili kupunguza uhaba wa Madaktari nchini Kenya. Mheshimiwa Rais alikubali ombi hilo.

"Machi 18, mwaka huu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ilitangaza nafasi hizo za ajira kwa Madaktari wa Tanzania kwenda kufanya kazi nchini Kenya. Maombi hayo yalipokelewa ambapo hadi Machi 27, mwaka huu ambapo jumla ya maombi takribani 496 yaliwasilishwa," alisema.


alisema baada ya kufanya uchambuzi wa maombi haya ilibainika kuwa, Madaktari 258 walikidhi vigezo vilivyotakiwa kwenda kufanya kazi nchini Kenya. Baadhi ya vigezo hivyo ni pamoja na:
Uhakiki wa vyeti vya taaluma na vyeti vya Sekondari, Chuo alichosoma na mwaka wa kuhitimu masomo, Sehemu alikofanya mafunzo ya vitendo (Intership) na mwaka wa kuhitimu mafunzo hayo.

https://www.broadnotes.com/news/story-images/imgm/69.jpgUzoefu wa kazi, Umri wa mwombaji usizidi miaka 55, Usajili wa mwombaji katika Baraza la Madaktari la Tanganyika, Asiwe mtumishi wa Umma, Hospitali Teule za Halmashauri na Hospitali za Mashirika ya hiyari wanaolipwa mishahara na Serikali.

"Wakati Serikali ya Tanzania ikiendelea kukamilisha utaratibu wa ajira za Madaktari wake nchini Kenya ikiwa ni pamoja na kutangaza nafasi hizo za kazi na kufanya uchambuzi wa maombi ya kazi, kuandaa Hati ya Makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Kenya kuhusu ajira hizo za Madaktari na Mkataba wa Ajira kwa Madaktari hao, wananchi (Madaktari) watano wa Kenya waliwasilisha pingamizi Mahakamani kuitaka Serikali ya nchi yao kusitisha kuajiri Madaktari kutoka Tanzania. 



"Kwa kuwa ratiba ya utekelezaji wa ajira hizi za Madaktari ilikubalika na pande zote mbili kuwa iwe imekamilika ifikapo tarehe 6 Aprili, 2017 na kuwa Madaktari hao wawe tayari kusafiri kwenda nchini Kenya kati ya tarehe 6-10 Aprili, 2017 na kwa kuwa hadi tarehe ya taarifa hii Mahakama nchini Kenya haijaondoa pingamizi lililofunguliwa kuhusu ajira za Madaktari wa Tanzania nchini Kenya," alisema.

Comments

Popular posts from this blog

SERIKALI YAREJESHA KAMBI TANO ZA JKT ZILIZOKUWA ZIMESITISHA MAFUNZO YA JESHI.

BELENG’ANYI, MBUNIFU MWENYE MALENGO YA KUTENGENEZA MGODI WA KUFUA UMEME.

WAKULIMA WA ZAO LA VITUNGUU IRINGA WATELEKEZA MASHAMBA.