CUBA IKO TAYARI KUTUMIA UTAALAMU NA FEDHA, KUONA ZANZIBAR INAFIKIA MAENDELEO.
Balozi
Mpya wa Cuba Nchini Tanzania Profesa Lucas Domingo Hernandez
Polledo Kushoto akisalimiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi
Seif Ali Iddi alipofika kujitambulisha rasmi hapo Vuga Mjini Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimkabidhi zawadi ya Mlango Balozi Mpya wa Cuba
Nchini Tanzania Profesa Lucas Domingo mara baada ya kumaliza mazungumzo yao.
Balozi Seif kati kati akiwa
katika picha ya pamoja na Mtaalamu wa Benki ya Dunia anayesimamia Kampuni ya
MIGA Bwana Yasumitsu Himeno wa kulia yake baada ya kufanya
mazungumzo Ofisini kwake kuhusiana na miradi ya Uwekezaji.
Na Mwandishi wetu, Zanzibar
JAMHURI ya Cuba imesema iko tayari
kutumia Utaalamu, Maarifa, Uzoefu na
fedha ili kuona Zanzibar inafikia maendeleo makubwa ya Wananchi
wake Kiuchumi kama ilivyofikia Nchi hiyo.
Balozi Mpya wa Cuba Nchini Tanzania,
Profesa Lucas Domingo Hernandez Polledo, alisema hayo wakati wa mazungumzo yake
na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi, alipofika
kujitambulisha rasmi hapo Vuga Mjini Zanzibar.
Profesa
Domingo alisema Cuba haina sababu ya kutoiunga mkono Zanzibar
katika harakati zake za kuimarisha uchumi kutokana na Historia ya muda mrefu
iliyopo baina ya Visiwa hivyo.
“Wananchi wa Jamuhuri ya Cuba tayari wameshaonyesha ukarimu mkubwa kwa
wenzao wa Zanzibar na natolea mfano
mafungamano ya Sekta ya Afya yalivyoimarika na kupata mafanikio makubwa hasa
kilipoanzishwa Chuo cha Madaktari
kinachosimamiwa na wataalamu wa Nchi hiyo,”alisema na kuongeza
“Wakati umefika kwa Mawaziri wa pande
hizi mbili rafiki kukaa pamoja kujadili namna viongozi hawa wanavyoweza
kushirikiana katika mambo yanayoonyesha kufanana katika utekelezaji wa pamoja,”
Alisema vikao hivyo vinaweza kuibua
mambo ya msingi ndani ya sekta ambazo kwa kiasi kikubwa zinaweza kusaidia
kwenye miradi mbalimbali ikiwamo Kilimo.
Pia amemuahidi, Makamu wa Pili wa Rais
wa Zanzibar kwa kipindi chake cha utumishi wa Kidiplomasia atazingatia zaidi kuimarisha uhusiano wa
Kihistoria wa pande hizo mbili.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
ameendelea kuishukuru Serikali ya Jamuhuri ya Cuba kwa juhudi inazochukuwa za
kuiunga mkono Zanzibar katika Sekta ya Afya ambayo tayari imeshazalisha
Madaktari wazalendo wasiopungua 50 kupitia Chuo cha Madaktari kinachosimamiwa
na Wataalamu wa Nchi hiyo.
Alisema moja ya fanikio kubwa
lililopatikana na ubanaji wa matumizi ya Serikali ambayo mwanafunzi Mmoja wa
kada ya Udaktari angelazimika kulipitia masomo yake kwa zaidi ya Dola za
Kimarekani 17,000 elfu.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikutana kwa mazungumzo na Ujumbe wa Wataalamu
wa Benki ya Dunia wanaojishughulisha na kusimamia miradi ya uwekezaji kupitia
Kampuni ya MIGA yenye Makao Makuu yake Nchini Japan.
Mazungumzo hayo ambayo pia
yalimjumuisha Balozi wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Nchini Japan
Balozi Mathias Chikawe aliyeambatana na Ujumbe huo yalifanyika Ofisini kwake
Vuga Mjini Zanzibar.
Bwana Yasumitsu alisema ipo miradi mingi
iliyoanzishwa katika Mataifa mbali mbali yenye uwanachama wa Benki ya Dunia
ambayo hupata mikopo chini ya Makampuni yanayodhaminiwa na Benki hiyo
yanayotozwa gharama za asilimia 50% ya mradi wanaoutekeleza.
Alitoa mifano ya miradi hiyo kuwa ni
pamoja Hospitali kubwa zenye uwezo wa kuhudumia wagonjwa katika Mikoa Mikoa na
Miji Mikubwa, majengo ya Vyuo Vikuu, Viwanja vya Ndege, miradi ya Ulinzi na
hata miuondombinu ya Bara bara.
Naye, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif ameushauri Uongozi wa Kampuni hiyo ya MIGA kuangalia
uwezekano wa kuunga mkono Mpango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wa kutaka
kuziimarisha Hospitali Mbili za Mikoa ya Kukisini na Kaskazini za Kisiwa cha
Unguja.
Comments
Post a Comment