WANACHAMA WATATU WA MAZOMBE SACCOS WAFUKUZWA UANACHAMA.

 Na Mwandishi Wetu, Ilula

CHAMA   cha ushirika cha akiba na mikopo cha Mazombe Saccos Ltd,kilichopo kwenye mji mdogo wa Ilula wilayani Kilolo mkoani Iringa kimewafukuza wanachama wao watatu akiwamo makamu mwenyekiti wa chama hicho  Ephrem Mgao kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo uchochezi.

Aidha,waliosimamishwa  uanachama huo ni Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho, Ephrem Mgao kwa sababu ya uchochezi,Ezekiel Mkusa na Rehema Myega ambao wote wawili walikuwa wamepoteza sifa za fungamano la chama.

Uamuzi huo umekuja mwishoni wa wiki kwenye mkutano mkuu wa 15 wa chama  hicho ambapo Mwenyekiti wa chama hicho, Yohana Mwemutsi alisema kuwa walipata taarifa kutoka kwa wanachama wenye nia njema na chama hicho kwamba kuna mtu anatoa taarifa za uchochezi juu ya chama hicho.

“Tulifanya uchunguzi  na tuligundua Mgao ndiye chanzo ,tuliamua kuitisha kikao kikao cha bodi na kumueleza kuwa yeye ndiye chanzo cha uchochezi katika chama na kumueleza sababu za kumsimamisha ujumbe wa bodi.”alisema Mwemutsi.

Mwemutsi alieleza kwenye mkutano huo sababu saba zilizopelekea kumfuta uwanachama Mgao kuwa ni amekuwa akipanga mbinu za uchochezi kwa baadhi ya wanachama kwa ajili ya kuvuruga mkutano mkuu wa mwaka 2016 na kwenda kinyume na maaazimio ya vikao vya bodi.

“Kutoa siri za mijadala ya vikao vya bodi kwa watu wasio husika wakiwamo wanachama na watumishi walioachishwa kazi huku yeye mwenyewe akiwa mshiriki na mpiga kura za kuwatoa watumishi hao kwa kuwa hata kura za kuwatoa zilizopigwa na wajumbe hakuna kura hata moja iliyosema watumishi hao waendelee na kazi,”alisema Mwemutsi

Pia  Kuwagonganisha wajumbe wa bodi,kamati ya usimamizi na watumishi kwa kutoa taarifa zisizo za kweli kwa kamati ya usimamizi kuhusiana na ubadhilifu ambapo aliwaambia mwenyekiti na meneja wamekuwa wakijilipa fedha kinyume na utaratibu kitu ambacho sio kweli.

Alisema Kuituhumu bodi kwa baadhi ya wanachama kwa kusema kuwa bodi hiyo iliwahi shawishika kugawana fedha za uzio wa ujenzi na kwamba yeye ndiye aliyezuia zoezi hilo,kitu ambacho si kweli ila ilikuwa ni mbinu ya ya kuichafua bodi na uongozi ili isiaminike kwa wanachama na hatimaye wanachama wakose imani na bodi ili apate nafasi ya kuchaguliwa kuwa mwenyekiti na hatimaye kuwafukuza baadhi ya watumishi asio wataka yeye akiwamo meneja wa chama.

Aliongeza kuwa sababu nyingine ni kuwa ni vikao vya siri maeneo tofauti tofauti na wanachama akishirikiana na aliyekuwa mlinzi wa Mazombe Saccos ambaye naye aliachishwa kazi kwa ajili ya kuwapanga wanachama kuuliza maswali huku akiwa amechapisha vipeperushi vyenye maswali hayo na kuwapa watu anaowaamini kuwa wana uwezo wa kuuliza maswali kwa lengo la la kuwaaminisha wanachama kuwa bodi waliyonayo haifai pamoja na meneja,watu hao alioshirikiana nao majina wanayo na ushahidi wa kutosha kuthibitisha jambo hilo.

Nyingine ni kuwahamasisha watumishi walioachishwa kazi kutolipa upotevu wa fedha waliosababisha kwa kufanya nao vikao pamoja na kufanya uchochezi kwa kupeleka kwa ofisa ushirika maneno ya uongo kuhusiana na upotevu wa fedha uliosababishwa na aliyekuwa karani wa fedha kwa kumwambia ofisa ushirika kuwa aliyekuwa karani wa fedha anapigwa vita na baadhi ya watumishi wenzake pamoja na wajumbe wa bodi,ambapo ofisa ushirika aliye hama Biezery Malila aliwapatia taarifa hizo kwamba mjumbe mwenzao ni chanzo . 

Hata hivyo Mgao alipewa nafasi ya kujitetea ambapo aliwaeleza wajumbe wa bodi kuwa yeye hahusiki na yote yanayosemwa ni majungu na baada ya kuendelea kumhoji kwa kina alikiri na kusema kuna baadhi ya mambo alihusika na mengine hahusiki ambapo wajumbe walimpa nafasi ya kukanusha baadhi ya amambo aliyoyasema. 

“Inawezekana kuna mahali niliteleza  kwa bahati mbaya hivyo akisamehewa ataenda kuwatuliza wanachama aliyowaeleza na kuchafua hali ya chama.”alisema Mgao.

 Kitendo cha kufanya uchochezi huo ni kinyume na maadili ya viongozi pia ni ukiukwaji wa misingi ya sheria ya vyama vya ushirika no.6 ya mwaka 2013,kanuni za vyama vya ushirika za mwaka 2015 kifungu no.51(M) na masharti ya chama.

Baada ya mwenyekiti kutaja sababu hizo na mtuhumiwa kukana kwa pamoja bodi na wajumbe waliokutana kwenye mkutano mkuu waliamua kumfuta uanachama pamoja wengine wawili ambao walipoteza sifa za fungamano la chama.

 Kwa upande wake Mrajis Msaidizi wa Mkoa wa Iringa John Kiteve alikubaliana na ushauri uliotolewa na wanachama na kuahidi kushirikiana na uongozi waSaccos hiyo kuhakikisha Mgao anavuliwa nyadhifa zake zote.

Akizungumzia lengo la chama hicho Meneja wa Mazombe Saccos Long'ino Ngwada alisema ni kuboresha utendaji kazi wa chama kwa kuwafikia wananchi wengi wa tarafa ya mazombe,kutoa gawio kwa wanachama.

Pia kuendeleza na kuimarisha mahusiano na mashirika,taaisi za kifedha ili kupata mtaji na vitendea kazi ,kutoa riba juu ya amana za wateja na wanachama,kutoa elimu ya vvu na ujasiriamali kwa wananchi ambapo hadi kufikia sasa saccos hiyo ina jumla ya wanachama 1677.


Comments

Popular posts from this blog

SERIKALI YAREJESHA KAMBI TANO ZA JKT ZILIZOKUWA ZIMESITISHA MAFUNZO YA JESHI.

BELENG’ANYI, MBUNIFU MWENYE MALENGO YA KUTENGENEZA MGODI WA KUFUA UMEME.

WAKULIMA WA ZAO LA VITUNGUU IRINGA WATELEKEZA MASHAMBA.