WAJAWAZITO WATAKIWA KUWAHI HOSPITALI WANAPOONA DALILI ZA KUJIFUNGUA.
Na Ramadhani Ali/Maelezo Zanzibar .
MAMA wajawazito wameshauriwa wanapoonyesha dalali za kuwa tayari kujifungua
wanatakiwa kuwahishwa Hospitali ama vituo vya afya mara moja bila ya kupewa
dawa za aina yoyote majumbani kwani ni hatari kwa afya zao.
Mwenyekiti wa Baraza la
Wakunga na Wauguzi Zanzibar, Amina Abdulkadir Ali, ameeleza hayo katika mkutano
na waandishi wa habari ikiwa ni maadhimisho ya siku ya Wakunga
Dunia katika Ukumbi wa Wizara ya Afya Mnazimmoja Zanzibar.
Alisema kumuwahisha mzazi
katika kituo cha afya mapema kunarahisisha kupata huduma kwa haraka na iwapo
anatatizo linalomkabili kujulikana mapema na kupatiwa ufumbuzi katika hatua za
awali.
Amina alisema huduma za mama wajawazito na watoto wachanga
zimeimarishwa katika vituo vingi vya afya vijijini na hakuna haja kwa mama wajawazito
kulazimisha kujifungulia Hospitali kuu ya Mnazimmoja.
Amewashauri kuvitumia vituo
vya afya vilivyokaribu nao na iwapo kutatokea tatizo kubwa ambalo haliwezi
kushughulikiwa katika kituo kidogo litapelekwa Hospitali kuu ya Mnazimmoja.
Alisema Baraza la Wauguzi na
Wakunga limeandaa mwongozo wa maadili kwa wauguzi na wakunga ambao unatakiwa
kufuatwa na wafanyakazi wa kada hizo kwa lengo la kuondoa malalamiko kutoka kwa
wananchi.
Amesisitiza umuhimu wa
wanaume kutoa upendo wa karibu kwa wake zao wakati wa ujauzito na wakati
wa kujifungua na hivi sasa zimewekwa wodi maalum katika Hospitali ya Mnazimmoja
zinazoruhusu wanaume kuwepo wodini wakati wake zao wanapojifungua.
Muuguzi Mkuu Kiongozi wa
Wizara ya Afya, Mussa Rashid Musaa, alisema vifo vya mama wajawazito wakati wa
kujifungua na watoto wachanga wakati wa kuzaliwa vimepungua kutokana na
kuimarishwa kwa huduma muhimu katika wodi za wazazi.
Alisema takwimu zinaonyesha
kuwa katika mwaka 2007 kila akinamama laki moja waliofika vituo vya afya kwa
ajili ya kujifungua 473 walifariki ambapo mwaka jana akinamama
waliofariki wakati wa kujifungua walikuwa 117.
Kwa upande wa watoto wachanga
amebainisha kuwa mwaka 2008 watoto waliofariki wakati wa kuzaliwa na mara baada
ya kuzaliwa walikuwa 31 kati ya watoto 1000 na mwaka jana walikuwa watoto 15
kati ya watoto 1000.
Hata hivyo amekiri kuwa idadi
ya vifo hivyo bado ni kubwa na Serikali inaendelea na juhudi za kuhakikisha
vifo vya mama wajawazito na watoto wachanga vinapungua kwa kuimarisha huduma
katika wodi hizo.
Kaulimbiu ya maadhimisho ya
siku ya Wakunga Duniani mwaka huu ni wakunga, akinamama na familia ni washirika
wa kudumu.
Mwenyekiti
wa Baraza la Wauguzi na Wakunga Zanzibar , Amina Abdulkadir Ali akizungumza na
waandishi wa habari katika Ukumbi wa Wizara ya Afya Mnazimmoja kuelekea
siku ya Wauguzi Duniani Mei tano.
Mwenyekiti
wa Jumuiya ya Wauguzi Zanzibar Valeria Rashid Haroub akitoa ufafanuzi wa
masuala ya waandishi wa habari kwenye mkutano wa kuelekea maadhimisho ya siku
ya wauguzi Duniani. Mkutano uliofanyika Wizara ya Afya Mnazimmoja.
Mwandishi
wa habari Sebetuu Amour wa Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) akiuliza swali
wakati wa mkutano wa Mwenyekiti wa Baraza la Wauguzi Zanzibar kuelekea kilele
cha maadhimisho ya siku ya wakunga duniani.
PICHA NA MAKAME MSHENGA- MAELEZO ZANZIBAR.
Comments
Post a Comment