VIONGOZI WANAOFICHA MATUKIO YA UKATILI DHIDI YA WATOTO KUCHUKULIWA HATUA.

Na Mwandishi Wetu, Mufindi

MKUU wa Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa, Jamhuri William amewatahadharisha viongozi na watendaji vijiji na kata kuwa atawachukulia hatua kali za kisheria kutokana na tabia zao za kuficha matukio ya ukatili dhidi ya watoto.

Mkuu huyo wa wilaya ametoa onyo hilo mjini Mafinga kwenye mkutano maalumu wa kuainisha mikakati ya kuimarisha ulinzi na usalama wa watoto wilayani humo.

Akiongea wakati wa mkutano huo ambao ulizikutanisha   taasisi mbalimbali ikiwamo jeshi la polisi,mahakimu wa mahakama ya wilaya, taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (Takukuru), jeshi la magereza na uhamiaji pamoja na viongozi wa dini na kimila.

 Alisema vitendo vya ukatili dhidi ya watoto vimefikia hatua ya kutovumilika na hatua zaidi zinapaswa kuchukuliwa ili kukomesha vitendo hivyo.

Aliongeza kuwa kwa mwaka huu  katika kipindi  cha miezi mitatu matukio 53 yanayohusu ukatili dhidi ya watoto yameripotiwa na katika kipindi cha mwaka 2013 hadi 2017 jumla ya matukio 153 ya ukatili dhidi ya watoto yameripotiwa na watuhumiwa kuchukuliwa hatua mbalimbali za kisheria ikiwamo kufugwa gerezani.

Alisema kuwa katika matukio hayo 53 yapo matukio 18 ya ubakaji,matukio saba ya ubakaji na mimba na matukio mawili ya ulawiti wa watoto na pia ipo tabia ya viongozi kwenye maeneo yao kuonesha tabia ovu juu ya kukwamisha jitihada zetu kwa kuficha matukio ya ubakaji,ulawiti na matukio ya ukatili juu ya watoto.

Pia  wanamifano halisi hivi karibuni yameripotiwa kutoka kijiji cha Nyololo,Ihegela na utagula na kijiji cha Nyololo tunajua mwenyekiti wa nyololo ameshirikiana na mtendaji kumficha na kumtorosha mbakaji wa watoto na kuishukuru vyombo vya dola kufanya kazi yao na kumtia nguvuni. 

Kwa upande wake hakimu mkazi Mfawidhi wa mahakama ya wilaya ya Mufindi Maua Hamduni alisema robotatu ya kesi zilizopo katika mahakama hiyo zinahusu ukatili dhidi ya watoto na changamoto kubwa inayowakabili ni ufinyu wa bajeti ikiwamo fedha za kuwawezesha mashahidi kufika mahakamani kutoa ushahidi pale wanapokosa nauli kutokana umbali wa sehemu wanaozotoka.

Hamduni alisema kuwa “Ukiangalia vizuri sheria ya mtoto utaona kwamba inamlinda zaidi mtoto mhalifu kuliko yule aliyetendewa na kupitia mikutano hii mtatusaidia watu wakilalamika mtasema jamani mahakimu adhabu walizotoa ndio ipo kwenye sheria hakuna adhabu nyingine na sisi kazi yetu ni kutekeleza sheria hutakiwi kwenda kinyume na sheria.”alisema Hamduni na kuongeza

“Kwa hiyo kama sheria inakuelekeza kwamba mtoto hatakiwi kufungwa gerezani unatakiwa kutoa adhabu hii unatakiwa kuitoa na sio kwenda kinyume na sheria inavyoelekeza.”alisema:

 Alisema kuwa sio siri hakuna asiyejua ofisi zote zinajulikana kwa sasa mafungu yanayokuja ni machache sana kwa mfano robo tatu ya kesi zilizopo kwenye mahakama ya wilaya ya mufindi ni za ubakaji na kila kesi unakuta zina mashahidi wanne au watano,na mafungu wanayoletewa hayakidhi uwezo huku akiwashukuru upande wa dawati kuwashauri hao watu kwenda mahakamani kwa kutumia nauli zao.

“Zamani tulikuwa tukiletewa Mil.10 za mashahidi lakini kwa sasa tunaletewa 400,000.”alisema

Alisema kuwa changamoto kubwa wanayokumbana nayo ni sababu ya kiuchumi,mashahidi kutofika mahakamani kutoa ushahidi,baadhi ya wazazi kutotoa ushirikiano.

Naye kaimu kamanda wa takukuru  wilaya ya Mufindi Peter Nkombe kama mtu anashindwa kutekeleza wajibu wa kuhakikisha anakamilisha ushahidi anatenda kosa.

Naye, Mery Tairo  kutoka dawati la jinsia wilaya Mufindi akizungumzia suala la  mimba alisema kuwa wamepokea kesi mbalimbali zinazohusuku ukatili wa watoto na jumla ya kesi 25 zinazohusu mimba kwa watoto wa shule ambapo kesi 12 zimefikishwa mahakamani na kesi 13 zipo chini ya upelelezi.

Kwa upande wake  Ofisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Mufindi, Elisha Nyamale  alisema  wamefanya kikao septemba 2015 tangu mwaka huo hadi machi 2017 jumla ya mashauri 36 ya watoto yametolewa hukumu,ambapo matukio 32 wameshinda kesi, jumla ya watuhumiwa 14,wamehukumiwa vifungo vya miaka 30 kila mmoja.

Alisema mtuhumiwa mmoja alihukumiwa kifungo cha miaka 60 jela wakati watuhumiwa wawili walihukumiwa kifungo cha maisha jela kwa makosa ya kulawiti watoto na watuhumiwa 12 wamehukumiwa kifungo cha nje wakati watuhumiwa watatu wamehukumiwa kwenda shule ya maadirisho Mkoani Mbeya.


Comments

Popular posts from this blog

SERIKALI YAREJESHA KAMBI TANO ZA JKT ZILIZOKUWA ZIMESITISHA MAFUNZO YA JESHI.

BELENG’ANYI, MBUNIFU MWENYE MALENGO YA KUTENGENEZA MGODI WA KUFUA UMEME.