MFUMUKO WA BEI WA TAIFA KWA MWEZI JUNI, 2017 UMEPUNGUA.
Mkurugenzi wa Sensa ya Watu
na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Ephraim Kwesigabo (kushoto) akizungumza
na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam wakati wa kutangaza Mfumuko wa
Bei wa Taifa wa mwezi Juni, 2017 ambao umepungua hadi asilimia 5.4 kutoka
asilimia 6.1 mwezi Mei, 2017. Kushoto kwake ni Meneja wa Takwimu za Bei na
Ajira, Ruth Minja.
Baadhi ya Waandishi wa
habari waliohudhuria katika Mkutano wa kutangaza Mfumuko wa Bei wa Taifa wa mwezi
Juni, 2017 uliofanyika jana jijini Dar es Salaam. Mfumuko wa bei umeonyesha
kupungua hadi asilimia 5.4 kutoka asilimia 6.1 mwezi Mei, 2017.
( PICHA NA
EMMANUEL GHULA)
Na,Veronica
Kazimoto.
MFUMUKO wa Bei wa Taifa kwa mwezi Juni, 2017 umepungua hadi asilimia 5.4
ikilinganishwa na asilimia 6.1 ilivyokuwa mwezi Mei, 2017.
Akizungumza na waandishi wa Habari jana jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa
Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Ephraim
Kwesigabo amesema Mfumuko wa Bei umepungua kutokana na kupungua kwa kasi ya
mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwezi Juni, 2017 ikilinganishwa na
kasi ya upandaji iliyokuwa kwa mwezi Mei, 2017.
“Mfumuko wa Bei wa mwezi
Juni, 2017 umepungua hadi kufikia asilimia 5.4 kutoka asilimia 6.1 mwezi Mei,
2017. Hii inatokana na kupungua kwa kasi ya upandaji wa bei za bidhaa na huduma
kwa mwezi Juni, 2017,” amesema Kwesigabo.
Amesema Mfumuko wa Bei unaopimwa
kwa kipimo cha mwezi umepungua kwa asilimia 0.1 ikilinganishwa na ongezeko la
asilimia 0.2 ilivyokuwa mwezi Mei, 2017.
Kwesigabo amesema Fahirisi
za Bei zimepungua hadi 109.10 mwezi Juni, 2017 kutoka 109.26 mwezi Mei, 2017. Amesema
Kupungua kwa Fahirisi za Bei kumechangiwa hasa na kupungua kwa bei za baadhi ya
bidhaa za vyakula.
Baadhi ya bidhaa za vyakula
zilizochangia kupungua kwa fahirisi ni pamoja na mahindi ambayo yamepungua kwa
asilimia 5.1, unga wa mahindi kwa asilimia 2.4, unga wa mihongo kwa asilimia
1.9, machungwa kwa asilimia 2.4, dagaa kwa asilimia 3.2, mbogamboga kwa
asilimia 5.7, maharage kwa asilimia 1.8 na viazi mviringo kwa asilimia 6.2.
Aidha Mfumuko wa Bei kwa
bidhaa za vyakula nyumbani na migahawani kwa mwezi Juni, 2017 umepungua hadi
asilimia 9.8 kutoka asilimia 11.8 mwezi Mei, 2017.
Uwezo wa Shilingi 100 ya
Tanzania katika kununua bidhaa na huduma umeimarika kidogo na kufikia Shilingi
91 na senti 66 mwezi Juni, 2017 ikilinganishwa na Shilingi 91 na senti 53
ilivyokuwa mwezi Mei, 2017.
Hata hivyo, Mfumuko wa Bei nchini Tanzania una
mwelekeo unaofanana na baadhi ya nchi nyingine za Afrika Mashariki kwa kuwa
Mfumuko wa Bei wa mwezi Juni, 2017 nchini Uganda umepungua hadi asilimia 6.4
kutoka asilimia 7.2 mwezi Mei, 2017; na nchini Kenya, Mfumuko wa Bei wa Mwezi
Juni, 2017 umepungua hadi asilimia 9.21 kutoka asilimia 11.70 mwezi Mei, 2017.
Comments
Post a Comment