MAHAKAMA YAMFUATA MANJI HOSPITALI, ASOMOMEWA MASHTAKA YA UHUJUMU UCHUMI
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana imelazimika kuhamishia shughuli zake katika Hospitali ya taifa ya Muhimbili kwa muda kumsomea mfanyabiashara Yusufali Manji (41), mashitaka ya uhujumu uchumi yanayomkabili.
Manji amesomewa mashtaka hayo katika Taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete iliyopo Hospitalini hapo mbele ya Hakimu Mkazi Mhe. Huduma Shaidi.
Katika kesi hiyo, Manji anashitakiwa pamoja na wenzake watatu, Meneja Rasilimali watu wa Kampuni ya Quality Group Ltd, Deogratius Kisinda (28), Mtunza stoo, Abdallah Sangey (46) na Thobias Fwere (43) mkazi wa Chanika, ambapo wote watatu wamesomewa mashtaka yao katika Mahakama hiyo kabla haijahamia hospitali ya Muhimbili kuanzia muda wa saa Tisa alasiri na kumalizika saa 16:41 (saa kumi na dakika arobaini na moja).
Mahakama ilifikia uamuzi wa kuhamia Muhimbili baada ya Manji kuwa amelazwa Hospitalini hapo akisumbuliwa na ugonjwa wa moyo na kulazimika kusomewa mashtaka yake akiwa kitandani.
Akisoma mashtaka hayo, wakili Mwandamizi wa Serikali, Tulumanywa Majigo amedai, Juni 30, mwaka huu huko Chang’ombe A wilayani Temeke jijini Dar es Salaam, washitakiwa wote kwa pamoja, walikutwa na askari polisi wakiwa na mabalo 35 ya vitambaa vinavyotumika kutengenezea sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) vyenye thamani ya milioni 192.5.
Imedaiwa kuwa, Julai Mosi mwaka huu, maeneo hayo hayo, washitakiwa wote walikutwa na askari polisi wakiwa na mabalo nane ya vitambaa vinavyotumika kutengenezea sare za JWTZ vyenye thamani ya milioni 44.
Aidha imedaiwa kuwa, Juni 30, washitakiwa hao walikutwa wakiwa na mhuri wa JWTZ ambao uliandikwa ‘’Mkuu wa Kikosi 121 Kikosi cha JWTZ’’ bila kuwa na uhalali kitendo kinachohatarisha usalama wa nchi.
Washtakiwa pia Pia wanadaiwa, kukutwa na mhuri uliokuwa umeandikwa ‘’Kamanda Kikosi 834 KJ Makutupora Dodoma bila kuwa na uhalali kitendo kinachohatarisha usalama.
Majigo aliendelea kudai kuwa mnamo Juni 30, mwaka huu maeneo hayo hayo, washitakiwa kwa pamoja walikutwa na mhuri ulioandikwa ‘’Commanding Officer 835 KJ, Mgambo P.o.Box 224 Korogwe isivyo halali.
Manji na mwenzake wamedaiwa kukutwa na gari lenye namba za usajili SU 383 mali waliyojipatia isivyo halali. Gari jingine wanalodaiwa kukutwa nalo washitakiwa ni lenye namba za usajili SM 8573 pasipo uhalali.
Washitakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa sheria ya uhujumu uchumi na ya usalama wa Taifa haijaipa mamlaka mahakama kusikiliza kesi hiyo.
Mawakili wa Serikali wakiongozwa na Mawakili waandamizi Mutalemwa Kishenyi, Nassoro Katuga na Majigo, walisema upelelezi wa shauri hilo haujakamilika na kwamba wamepata hati ya kupinga dhamana kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP).
Wakili Katuga alidai kuwa DPP anaomba ruhusa washitakiwa wasiruhusiwe kupewa dhamana kwa sababu wakiachiwa watahatarisha usalama na maslahi ya nchi. Pia alidai kwenye mashitaka ya kwanza na ya pili, mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kushughulikia masuala ya dhamana.
Hata hivyo, Wakili wa utetezi, Hudson Ndusyepo, alipinga hoja zilizotolewa na upande wa mashitaka kwamba mashitaka hayo yanaiondolea mahakama kufikiria suala la dhamana kwa washitakiwa.
Ndusyepo alidai upande wa mashitaka umekuwa na nia mbaya ya kuwasilisha hati ili kupinga dhamana na kudai kuwa kitendo hicho ni matumizi mabaya ya madaraka ambayo hawawatendei haki washitakiwa.
Hata hivyo, Hakimu Shaidi alisema kuwa masuala hayo yalitakiwa kuongelewa katika mahakama yenye mamlaka ambayo ni Mahakama Kuu na kwa sababu DPP hajaipa mamlaka mahakama hiyo kusikiliza kesi hiyo, hivyo hawezi kuzungumza chochote.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Julai 19, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa na washitakiwa watatu wamerudishwa rumande huku mshitakiwa Manji, amebaki chini ya uangalizi wa polisi na baadaye Magereza kwa kipindi chote atakachokuwa hospitalini hapo, na kuhamishiwa mahabusu baada ya kupata nafuu.
Comments
Post a Comment