ASKOFU MWAMAKULA AIOMBA SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WANAOTUMIA DINI KUWARUBUNI WATU.
Na Enles Mbegalo
ASKOFU
Mkuu wa Dayosisi Kuu ya Dar es Salaam na Mkuu wa Kanisa la Moravian la
Uamsho Tanzania (KMUT), Emmaus Mwamakula, amemuomba Rais John Pombe Magufuli,
kupitia Taasisi na vyombo vyake kuwachunguza na kuwachukulia hatua watu wote
wanaotumia dini katika kuwarubuni watu.
Akizungumza na mwandishi wa blog hii
leo, jijini Dar es Salaam, Mwamakula alisema afya za watu zitakuwa salama
endapo serikali itazuia uholela katika uendeshaji wa vikundi vya dini kwa kuhakikisha viongozi wa dini wanakuwa na mafunzo, maadili
na historia inayoeleweka.
Askofu Mwamakula alitoa wito
kwa watu wanaotapeliwa na watu wanaotumia kivuli cha dini kuanza kujitokeza
hadharani kwa kutoa taarifa katika vyombo vya sheria ili kuweza
kuzuia machafuko katika nchi kwa kutunza afya za watu.
“Ninaiomba serikali yetu kuhakikisha
kuwa watu wanaoongoza Taasisi za Dini wawe ni watu ambao historia zao zinajulikana
hasa kuhusiana na wapi watu hao walipata mafunzo yanayohusiana na shughuli zao,”
Alisema ifike mahali jamii ielewe kuwa
mambo ya imani yakiachwa yaendeshwe kiholela na watu ambao hawana mafunzo na uongozi thabiti
itakuwa hatari kubwa.
“Nchi
inapokuwa na watu wenye afya nzuri katika mambo haya matatu uchumi, usalama na ustawi wake unakuwa ni wa
uhakika kwani katika miaka ya hivi karibuni jamii yetu imeshuhudia watu ambao historia
ya mafunzo yao hayajulikani lakini
wamekuwa wakianzisha Taasisi za Dini huku uendeshaji wake ukiwa mikononi mwa
watu binafsi,”alisema Askofu Mwamakula na kuongeza
“ Ustawi wa jamii yeyote ile duniani
unategemea sana afya ya kiakili, kimwili na kiroho kwa wanajamii husika na
imani potofu zinaweza kuathiri uchumi, usalama na ustawi wa jamii,”
Pia Askofu Mwamakula alitoa mfano wa kuibuka kwa wingi wa vikundi vya dini ambavyo viongozi wao hutoa ahadi za kuwaponya watu watakaotoa fedha vitendo ambavyo hupelekea kuwafilisi wahanga.
Comments
Post a Comment